Veta Lindi yatoa mwarobaini wa ajira kwa vijana

Mkuu wa chuo cha Veta Lindi, Harry  Mnari akisoma taarifa ya chuo kwenye mahafali ya pili ya programu ya miezi mitatu yaliyofanyika jana Aprili 26, 2023

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema ili vijana wapate mikopo na waweze kujiajiri hawana budi kujiunga katika vikundi.

Lindi. Vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi stadi Veta mkoani Lindi wametakiwa kujiunga katika vikundi ili waweze kukopesheka na kujiajiri.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga wakati wa sherehe za mahafali ya pili ya programu ya miezi mitatu inayofadhiliwa na Taasisi ya ‘Employment and Skills for Development in Africa’ kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Ajira.

Ndemanga amewataka wahitimu hao wa awamu ya pili kujiunga katika vikundi ili iwe rahisi kukopesheka kupitia mikopo ya halmashauri na taasisi binafsi kulingana na mradi wanaokusudia kwani hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira katika soko.

“Watakaofanikiwa kuingia katika ajira isiyo rasmi, ni vyema niwashauri kuunda au kujiunga na vikundi vidogo vidogo ili kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za fedha,” amesema Ndemanga.

Mkuu wa Wilaya huyo amewasisitiza wahitimu hao kuziishi ndoto zao sanjari na kuchukua tahadhari dhidi ya makundi mabaya ili kuepuka kutumbukia kwenye ulevi, ngono zembe na matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa upande Mratibu wa Mradi wa Kukuza Ujuzi na Ajira kwa Vijana (E4D), Mawazo Mateje amesema  mpango  huo unasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana kwa kushirikana na wadau mbalimbali ikiwemo GTZ na Veta Lindi.

Mateje amesema kwa awamu ya kwanza  vijana  145 walihitimu na awamu pili 135, pamoja na  mafanikio hayo lakini wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa walimu na baadhi ya vijana kutokamilisha kozi.