VIDE0: Mawakala saba Chadema, NCCR wafukuzwa vituoni

Muktasari:

  • Wasimamizi wa uchaguzi kituo cha Pugu Mnadani kata ya Pugu wamewaondoa vituoni mawakala saba wa Chadema, NLD na NCCR Mageuzi kwa maelezo kuwa hawana barua za utambulisho wa mtendaji wa kata

Dar es salaam. Wasimamizi wa uchaguzi kituo cha Pugu Mnadani kata ya Pugu wamewaondoa vituoni mawakala saba wa Chadema, NLD na NCCR Mageuzi kwa maelezo kuwa hawana barua za utambulisho wa mtendaji wa kata.

Tukio hilo limetokea leo Jumapili Septemba 16, 2018 saa 8:30 asubuhi huku mamia ya wananchi wakiwa katika foleni ya kupiga kura kumchagua mbunge wa jimbo la Ukonga.

MCL Digital imeshuhudia mmoja kati ya mawakala hao, Gabriel Samson akiondolewa na polisi watano waliopo kituoni hapo ikiwa ni dakika chache baada ya kufika.

“Askari naomba uniondolee huyu mtu hapa, mwondoe tafadhali, nimesema hatukuhitaji hadi uwe na barua ya mtendaji wa kata,” amesikika akisema mmoja wa wasimamizi hao ambako polisi walitekeleza amri hiyo.

Akizungumzia kitendo hicho Samson amesema hujuma imeandaliwa mapema na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

“Tulipokula viapo tuliambiwa viapo na fomu zote tutazikuta kituoni, leo tunafika kituoni hapa tunaambiwa haturuhusiwi hadi barua na hati za viapo. Tunarudi ofisi ya mtendaji wa kata hayupo," amesema Samson akiwa na mawakala wengine sita wa NLD na NCCR Mageuzi.

Hata hivyo, kituoni hapo kulikuwa na mawakala wawili  wa vyama vya Sau na AFP, walioonyesha barua zao za utambulisho wa mtendaji wa kata.

 

Mawakala hao, Elick Mgasha (Sau) na Albert Modest (AAFP) wamesema hakukuwa na usumbufu wowote wakati wa kufuatilia barua hizo kwa mtendaji wa kata hiyo.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi kituoni hapo, Mustapha Zayumba amesema hakuna wakala aliyeruhusiwa kuingia kituoni hapo bila barua ya mtendaji wa kata.

"Hata mawakala wa CCM saba tumewaondoa, hawakuwa na barua ya mtendaji wa kata, wameondoka kuzifuata, hakuna wakala anayeonewa hapa ila utaratibu lazima ufuatwe, "amesema Zayumba.

Dakika chache baadaye lilionekana kundi la mawakala wa CCM waliojikusanya pembeni na walipohojiwa na MCL Digital wamesema wanafuatilia barua hizo.

Mawakala hao wa CCM ni Mwajuma Gobel, Salim Said, Nicodem Mganga, Jesca Roma, Upendo Ndomba na Kilopola Mohamed.