VIDEO: Adha ya daraja inavyowatesa wakazi Pwani, Dar

Muktasari:

  • Daraja hilo ambalo ni kiunganishi cha pande mbili kinategemewa hasa na wananchi wa kata ya Pangani ambao hununua mahitaji yao upande wa Kibwegere jijini Dar es Salaam.

Pwani. Wananchi wa kata ya Pangani Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani na Kibwegere Wilayani Ubungo, Dar es Salaam, wameiomba Serikali kuwatengenezea daraja,  ili kuondokana na adha wanayoipata kipindi cha mvua na kusababisha kukatika kwa mawasiliano.

Daraja hilo ambalo ni kiunganishi cha pande hizo, mbili kinategemewa hasa na wananchi wa kata ya Pangani ambao hununua mahitaji yao upande wa Kibwegere jijini Dar es Salaam.

Mbali na ununuzi wa bidhaa pia daraja hilo ambalo lilisombwa na maji Novemba, mwaka jana, hutumiwa na wanafunzi wanaosoma shule zilizopo Kibwegere pamoja na huduma nyingine za kijamii ikiwemo za afya.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema inaponyesha mvua mto huo hufurika na kusababisha kukatika mawasiliano na kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii.

Adha ya daraja inavyowatesa wakazi Pwani, Dar

Saimon Warioba mkazi wa Mtaa wa Lumumba kata ya Pangani amesema adha hiyo ni ya muda mrefu zadi ya miaka 12 kila mvua zinaponyesha husababisha mafuriko makubwa.

Amesema nyakati za mvua wanafunzi wanaotoka mkoa wa Pwani hususani kata ya Kibwegere ambao hutegemea shule zilizopo Wilaya Ubungo kwenye kata ya Kibamba, hukumbana na adha kubwa.

“Adha hii ni ya muda mrefu ukiacha mto huu kuwa na mamba kipindi cha mvua, watu husombwa na maji, tumepiga kelele sana, walikuja watu wakachukua vipimo (vya ujenzi wa daraja) lakini hadi sasa hatujaona utekelezaji wake,” amesema Warioba.

Amesema wanafunzi ni miongoni mwa watu wanaosombwa na maji na wengine husababisha wapoteze maisha.

Hivyo, amesema wanaiomba Serikali sasa itazame namna ya kuwanusuru kwa sababu hata vivuko vya kienyeji wanavyovijenga haviwasaidii kwa sababu si salama.

“Tarura (Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini) walishawahi kuja wakaangalia lakini hatujui utekelezaji uko wapi, tunahitaji daraja kubwa ili mtaa wa Lumumba tuweze kupata mawasiliano na kata ya Kibwegere mkoa wa Dar es Salaam,” amesema mkazi huyo.

Amesema asilimia kubwa ya mahitaji yao huyapata Ubungo mkoani Dar es Salaam.

“Lakini kulingana na miundombinu ilivyo, hata pikipiki ni changamoto kupita hapa, vijana hujitolea lakini mvua inaponyesha tabu ipo palepale,” amesema.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Lumumba iliyopo Kibaha, Mwamtoro Mshuti amesema walimu wengi wa shule hiyo wanaishi Kibwegere na daraja hilo hulitumia kufika kazini.

“Mvua ikinyesha na daraja likajaa, hatuwezi kwenda kazini na ikitukuta kazini hatuwezi kurejea nyumbani au la huwa tunatumia njia nyingine ambazo ni mbali sana,” amesema Mshuti.

Hata hivyo,  mwalimu huyo amesema mbali na walimu hata mahudhurio ya wanafunzi hupungua kwa sababu wengi wao hawaendi shuleni.

Kwa upande wake,  mwanafunzi Fatuma Mohamed anayesoma shule ya Sekondari Kiboheri ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwajengea daraja hilo sasa.

“Mvua ikinyesha tunazunguka umbali mrefu na wakati mwingine hatuendi shuleni kabisa, tukienda tunaogopa kwa sababu wapo wenzetu wameshasombwa na maji,” amesema mwanafunzi huyo.


Mwenyekiti azungumza

Licha ya kero hizo wanazozipata wananchi, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibwegere, Humphrey Mtili amesema daraja hilo ni kiungo muhimu kwa wananchi hasa kwa Mkoa wa Pwani kwa kuwa shughuli zao nyingi za kiuchumi hutegemea kuzitekeleza kutokea Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema Mkoa wa Pwani wanapaswa kugharamia daraja hilo licha ya kuunganisha mikoa miwili.

“Kama ni suala la bajeti inabidi liwe shirikishi, watu wa upande wa pili wamekuwa wakitegemea mahitaji yao huku inabidi wakae chini baada ya kujadiliana watushirikishe ili tujue ni namna gani na sisi tutashiriki kuchangia”amesema Mtili.

Akizungumzia mkakati uliopo Diwani wa kata ya Pangani Agustino Mdachi,  amesema mpango wa dharura upo ili kunusuru hali iliyopo wakati huu wa mvua.

Amesema daraja hilo ni la muhimu kwa kuwa wananchi wa mkoa wa Pwani wamekuwa wakitegemea kununua bidhaa zao mkoa wa Dar es Salaam, ndio maana kilitengenezwa kivuko ambacho kililisombwa na maji.

“Kuna mkakati unaendelea ili kupata kivuko cha muda kwa ajili ya kupita bajaji na pikipiki kitakachogharimu Sh10 milioni, Serikali ilishafanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya daraja la kudumu, baada ya wiki mbili tunaweza kutoa taarifa tumefikia wapi,”alisema Mdachi.


Kauli ya Mkuu wa Mkoa Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema baada ya mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni, wamekuwa wakishirikiana na mamlaka nyingine kurejesha miundombinu katika hali ya kawaida.

Amesema kila jambo linahitaji bajeti, hivyo kwa kushirikiana na Tarura na Halmashauri wataangalia ni namna gani wataweza kutatua changamooto hiyo.

“Ni kweli baada ya mvua ipo baadhi ya miundombinu iliyoharibika ambayo ni pamoja na hilo daraja, tumekuwa tukishirikiana na wenzetu wa Halmashauri na Tarura kuangalia ni namna gani ya kuirejesha, pamoja na yote hayo kila kitu kinahitaji bajeti, kwa hiyo tunajipanga kibajeti ili tuanze utekelezaji wa ujenzi,” amesema Kunenge.


Kauli ya Tarura Dar

Kwa upande wakem  Meneja wa Tarura Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga amekiri kuwa wataalamu wake tayari walishalifanyia  tathimini daraja hilo licha ya kuwa linatumika zaidi na wakazi wa Mkoa wa Pwani.

Hata hivyo, amesema kwa sasa wanaendelea na mazungumzo ya kuona namna gani watashirikiana kulijenga daraja hilo.