VIDEO: Ali Kiba ategua kitendawili, afunga ndoa Mombasa

TAZAMA ALI KIBA ALIVYOFUNGA NDOA MSIKITI WA UMMUL KULTHUM MOMBASA

Muktasari:

Ndoa ya Kiba na Amina ilifungishwa na Sheikh Mohammed Kagera jana alfajiri katika msikiti huo.

Mombasa. Hatimaye kitendawili cha ndoa ya mwanamuziki Ali Kiba kimeteguliwa jana baada ya kufunga ndoa na Amina Khaleef katika Msikiti wa Ummul Kulthum uliopo eneo la Kizingo jijini Mombasa.

Awali, kulikuwa na sintofahamu ya ndoa hiyo kwa takribani wiki mbili kwamba huenda ilishafungwa na kwamba kilichobaki ni sherehe ambayo ingefanyika hapa nchini Kenya.

Ndoa ya Kiba na Amina ilifungishwa na Sheikh Mohammed Kagera jana alfajiri katika msikiti huo.

Mbali na familia ya Kiba, watu mbalimbali maarufu walihudhuria sherehe hiyo wakiwamo viongozi wake wa Rock Star 4000, mtangazaji maarufu wa Kenya, Gaddafi, mwanamuziki Ommy Dimpoz. Awali, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alitajwa kuwa angekuwa mmoja wa wageni, lakini ilielezwa baadaye kuwa asingeweza kufanya hivyo kutoka na kubanwa na majukumu mengine.

Baada ya kisomo cha ndoa, uliwadia muda wa kushikana mkono na walii na kumuozesha rasmi msanii huyo mkali wa kibao cha ‘Seduce Me’.

Katika hatua hiyo, Kiba akatamka: “Mimi Ali Saleh Kiba nimekubali kumuoa Amina Khalef kwa mahari tuliyosikilizana na ikitokea sababu ya kuachana tuachane kwa wema.” Baada ya kutoka msikitini, mfululizo wa sherehe ulifuata zikianzia nyumbani kwa Abu Joho ambaye ni ndugu wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho eneo la Kizingo na baadaye mlo wa mchana katika jumba la kifahari linalomilikiwa na Gavana Joho eneo la Kaunti ya Kilifi. Ilipofika saa 12 jioni, sherehe hizo za harusi zilihamishiwa katika ukumbi wa Diamond Jubilee ambako wageni zaidi ya 500 walihudhuria.

Harusi ya Kiba imefuatiliwa tangu zilivyoanza fununu kutokana na msanii huyo kuwa msiri.

Mbali na hilo, pia wengi walitaka kujua ni nani hasa anamuoa baada ya miaka ya hivi karibuni kuwahi kuwa na uhusiano na Jokate Mwegelo, aliyewahi kuwa mshindi wa pili wa mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2006.

Pia harusi hiyo imekuwa na mvuto baada ya kuelezwa kuwa itarushwa mubashara na kituo cha televisheni cha Azam ikiwa ni tukio la kihistoria nchini.

Jana, mama mzazi wa mke wa Kiba, Asma Said alisema amefurahi binti yake kuolewa na msanii huyo na hakutegemea hilo lingetokea katika familia yake.

“Amina ni binti yangu wa mwisho kati ya watoto wangu wanne, nimefurahi ameolewa na Ali kiba kutoka Tanzania, masuala ya ndoa Mungu ndio hupanga kwa hiyo tumempokea kwa furaha,” alisema.