VIDEO: Azam yapewa leseni kuonyesha chaneli za ndani bure

Naibu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace
Muktasari:
Serikali imeikabidhi televisheni ya Azam leseni ya kuonyesha chaneli za ndani bure
Dodoma. Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye amelieleza Bunge leo Jumanne Mei 14, 2019 kuwa kituo cha televisheni cha Azam jana Jumatatu kimepokea leseni ya kuonyesha chaneli za ndani bure.
Pia, Nditiye amesema katika kipindi cha miezi saba watajenga mfumo wa kurusha chaneli hizo, hivyo wananchi wanapaswa kuvuta subira.
Naibu waziri ametoa kauli hiyo akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, aliyehoji ni kwa nini Azam wananyimwa haki ya kuonyesha channel za ndani bure.
"Je, Serikali haioni kuwanyima haki hiyo wakati wengine wamepewa ni kukiuka ibara ya 18 ya katiba ambayo inatoa haki ya kupata habari, lakini hata Rais wetu anatumia Azam kurusha matangazo yake hivyo tungejitangaza hadi nje," ameuliza Shangazi.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Nyamagana (CCM), Stanslaus Mabula, aliuliza Serikali iwapo haioni kupitia TCRA kuwafungia local channels (chanel za ndani) baadhi ya ving'amuzi ikiwamo Azam TV, DSTV na vingine imewanyima wananchi fursa ya kupata habari.
Naibu waziri amesema Serikali inatambua umuhimu wa wananchi kujua mambo yanayoendelea, hivyo imetoa leseni zenye masharti tofauti.
Amesema kwa sasa matangazo ya umma yanarushwa na TBC1 na TBC3 maarufu safari channel.
Kwa mujibu wa Nditiye, kampuni zinazomiliki ving’amuzi vya DSTV, Zuku na Azam hayakustahiki kutoa huduma ya kubeba chaneli za ndani zisizolipiwa kutokana na masharti ya leseni zao.
Amesema Serikali imefanya jitihada ya kukaribisha maombi ya leseni ya kubeba maudhui ya chaneli za ndani kutoka kwa wanaohitaji kutoa huduma ikiwamo kampuni hizo ili ziweze kupata leseni stahiki.