VIDEO: Diwani aliyepatikana kwa Ashura kufanyiwa sherehe

Friday June 24 2022
diwanipiic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge amesema leo wanatarajia kumfanyia sherehe ya kumkaribisha Diwani wa Kawe (CCM), Mutta Rwakatare ambaye alipotea mwanzoni mwa mwaka huu.

Diwani Rwakatare alipatikana Machi eneo la Tabata akiwa nyumbani kwa mwanamke alijulikana kwa jina la Ashura na leo Ijumaa Juni 24,2022 alihudhuria kikao hicho jambo lililoamsha shangwe kutoka kwa wenzake.

Mutta aliyekuwa amevalia suti ya ‘dark blue’ yenye michoro ya drafti aliingia ukumbini saa 7:22 mchana hali iliyowafanya madiwani waliokuwa ukumbuni hapo kumshangilia.

Mara baada ya kuingia diwani huyo ambaye ni mtoto wa marehemu Mchungaji Getrude Lwakatare, alikwenda moja kwa moja kwenye viti walivyokaa madiwani na kusalimiana nao kwa kuwashika mikono na wengine kuwakumbutia.

Baada ya hapo alikwenda kuchukua joho lake sehemu ambayo majoho ya madiwani yalikuwa yamewekwa na kulivaa na  kisha kukaa kwenye kiti kilichopo   kona upande wa kushoto wa ukumbi.

Advertisement

Meya amkaribisha

Akifungua kikao cha Baraza la Madiwani, Meya wa Manispa ya kinondoni Songoro Mnyonge, alitambua uwepo wa diwani huyo na kueleza kuwa wamefurahi kumuona tena.

"Tunashukuru mwenzetu Diwani Mutta aliyekuwa ametoweka na mimi kutangaza kwenye kikao kama hiki kuwa tunamtafuta lakini baadaye akarejea, tayari ametuahidi kuwa hatapotea tena karibu sana Mheshimiwa Mutta,"amesema Mnyonge huku akipigiwa makofi na madiwani kwa kugonga meza.

Meya Myonge amesema leo watafanya sherehe ya kufurahia kurejea kwa diwani Mutta.

Advertisement