VIDEO: Dk Mwinyi atoa ujumbe baada ya kutangazwa mshindi

Muktasari:

Mara baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha urais Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Mwinyi amewataka Wazanzibari kuungana kuyaponya majeraha ya uchaguzi mkuu.

Dar/Unguja. Mara baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha urais Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Mwinyi amewataka Wazanzibari kuungana kuyaponya majeraha ya uchaguzi mkuu.

Katika uchaguzi huo Dk Mwinyi amepata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 ya kura zote.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Dk Mwinyi aliwashukuru wapiga kura wa Zanzibar, “natamka kuwa nimepokea kwa mikono miwili na moyo mkunjufu ridhaa ya Wazanzibar waliojitokeza jana kuamua kupitia sanduku la kura juu ya chama gani na mgombea gani apewe ridhaa ya kuongoza awamu ya nane ya Rais wa Zanzibar.”

Ameongeza, “wajibu ulioko mbele yetu ni kudumisha amani yetu. Uchaguzi sasa umekwisha, turudi tuwe kitu kimoja, tuponye madonda ya uchaguzi huu na tuijenge Zanzibar mpya.”

Pia, aliwaomba viongozi wa CCM kuwatuliza wananchi wayapokee matokeo.

“Wito kwa wana CCM wenzangu tusherehekee kwa staha bila kuwakwaza wenzetu. Hakuna ushindi wetu bila ushindani wao, tunawahitaji ili kushamirisha demokrasia yetu na mchakato mzima wa maendeleo,” amesema Dk Mwinyi.

Alikishukuru chama hicho kwa kumteua kugombea nafasi hiyo akiomba wanachama wenzake kuendelea kumpa ushirikiano.

“Mimi Hussein Mwinyi si bora kuliko CCM, ushindi huu ni wa wana CCM wote. Nafahamu kuwa CCM ina hazina kubwa ya wanachama wanaofaa kuongoza, lakini kiliniteua mimi kupeperusha bendera na hatimaye kufanikisha ushindi,” amesisitiza.