Kisebengo kizimbani akidaiwa kusafirisha heroini na kokeni

Mkazi  wa Mbezi jijini Dar es Salaam, Nasibu Kisebengo (aliyebeba mfuko) akiingia katika Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kwa ajili ya kusomewa mashtaka ya kisafirisha dawa za kulevya.

Dar es Salaam.  Mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam, Nasibu Kisebengo (44), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini na kokeni kinyume na sheria.

Kisebengo amefikishwa mahakamani hapo leo Jumanne Aprili 30, 2024 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Happy Mwakanyamale mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalloh.

Mwakanyamale amedai kuwa katika shtaka la kwanza, Kisebengo anatuhumiwa Februari 27, 2024 alikutwa eneo la Feri Tatavamba ndani ya Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam akisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini gramu 5.76.

Amedai kuwa, katika shtaka la pili mshtakiwa alikutwa eneo hilo na tarehe hiyo akituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya kokeni gramu 0.82.

Wakili huyo ameendelea kudai kuwa, Februari 28, 2024 mshtakiwa akiwa eneo la Mbezi Zone Makaranga ndani ya Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam alikutwa akisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini gramu 20.96.

Baada ya mshtakiwa kusomewa mashtaka hayo alikana kuhusika na tuhuma hizo, Wakili Mwakanyamale amedai kuwa hakuna dhamana kutokana na mashtaka anayetuhumiwa nayo.

Pia, amedai kuwa upelelezi bado unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo na kuangalia hatua ya upelelezi ilipofikia. Hakimu Swalo ameharisha kesi hiyo hadi Mei 14, 2024 kwa kutajwa.