VIDEO-Kamati Kuu CCM yakutana

Muktasari:

Kamati Kuu itapokea tathmini ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43.

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inakutana jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti Rais John Magufuli.

Kikao cha Kamati Kuu kinachofanyika leo Jumatatu Novemba 20,2017 kitafuatiwa na kingine cha Halmashauri Kuu ya Taifa kesho Jumanne Novemba 21,2017.

Taarifa iliyotolewa awali na Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM, Humphrey Polepole imesema vikao hivyo pamoja na mambo mengine vitakuwa na ajenda ya kupokea tathmini ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 ambao kampeni zake zinaendelea.

“Ajenda nyingine ya vikao hivi vya uongozi vya kitaifa itakuwa kupokea, kuchuja, kutoa mapendekezo na kufanya uteuzi wa mwisho katika ngazi ya mikoa na taifa katika chama na jumuiya zake kwa maana ya umoja wa vijana, wanawake na wazazi,” ilisema taarifa ya Polepole.

CCM sasa ipo katika mchakato wa uchaguzi wa ndani kuanzia ngazi ya shina mpaka taifa.