VIDEO: Katani awashukia Mawaziri Bashe, Mwigulu

Mbunge wa Tandahimba, Katani Katani akizungumza  wakati akichangia mjadala wa kamati za Bunge za kudumu Bungeni Dodoma. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Kauli ya Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba kuwa wabunge wasiokuwa na taaluma ya uchumi wakajadili mambo ya uganga wa kienyeji inaendelea kumtafuna Waziri huyo, baada ya Mbunge wa Tandahimba, Katani Katani kuibuka nayo bungeni.

Dodoma. Mawaziri wa Kilimo Hussein Bashe na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba viti vyao vimekuwa moto katika mkutano wa Bunge unaoendelea jijini hapa.

 Wawili hao wamekuwa wakitajwa mara nyingi na wabunge huku wengine walionekana kutoridhishwa na kinachofanyika ndani ya wizara zao.

Leo Februari 7, 2023 Mbunge wa Tandahimba Katani Katani (CCM) amewataja mawaziri hao kuwa wanachokifanya ni porojo.

Katani amemtaja Waziri Bashe kuwa amekuwa na maneno mengi lakini utendaji wake hauendani na anachokitamka.

VIDEO: Katani awashukia Mawaziri Bashe, Mwigulu

Amemtaja Waziri Bashe kwamba aliweka ahadi ya kuongeza uzalishaji wa pamba kufikia tani 700,000, akisema endapo waziri huyo atatekeleza hilo, yeye (Katani) yuko tayari kubaki jimboni kwake Tandahimba Mwaka 2025.

"Waziri Bashe acha porojo, hili litakutafuna. Miezi sita unasema hakuna mfumo wakati minara imejengwa nchi nzima, fanyeni tathimini," amesema Katani.

Amezungumzia deni lililozalishwa na Wizara ya Kilimo kwa wazabuni kuwa limefikia Sh80 bilioni ambalo limetengenezwa na bodi.

Akijibu tuhuma za bei ya mazao, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema hakuna namna ya kuwasaidia wakulima kupata bei nzuri ikiwa hakutakuwa na vyama vya ushirika vilivyo imara.

Bashe amesema hakuna njia itakayomuondoa mfanyabiashara wa mazao lakini akasema Serikali itakachofanya ni kupunguza gharama za uzalishaji lakini haitaingilia bei ya mazao ya wakulima.

Katika hatua nyingine Katani amemtuhumu Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba kwamba aliwatukana kwa kuwambia wakajadili masuala ya uganga wa kienyeji kitu ambacho hakina tija.

Kauli ya uganga wa kienyeji aliitoa Waziri Mwigulu Nchemba wiki iliyopita wakati akimjibu mbunge wa Kisesa Luhaga Mpin ambapo alimwambia, 'Wasio wachumi wakajadili mambo ya uganga wa kienye na kwenye uchumi this is my professional (hii ni taaluma yangu).”