VIDEO: Kesi ya Mdee yakwama, wakili aomba kupitia jalada

Muktasari:

Wakili wa upande wa mashtaka katika kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Tanzania, John Magufuli inayomkabili Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ameomba muda kwa ajili ya kupitia jalada.

Dar es salaam. Kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Tanzania, John Magufuli inayomkabili Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee imeshindwa kuendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam baada ya wakili kuomba kupitia jalada.

Wakili wa Serikali, Dhamiri Masinde amedai leo Jumanne Aprili 16, 2019 mbele ya  Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusikilizwa na shahidi yupo ila anaomba muda kwa ajili ya kupitia jalada.

"Kesi imekuja kwa ajili ya kusikilizwa, tunaye shahidi Abdi Chembeya, naomba muda kwa ajili ya kupitia jalada kutokana na wakili aliyekuwa anasikiliza kesi hii awali kuwa na majukumu mengine," amedai  Wakili Masinde.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai kuwa kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa leo, hivyo hana pingamizi kwa tarehe nyingine itakayopangwa. Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 24, 2019 kwa ajili ya kuendelea na usikilizaji.

Mpaka sasa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi katika kesi hiyo akiwamo mkuu wa Kituo cha Polisi Urafiki, Mrakibu wa Polisi (SP), Batseba Kasanga.

Katika kesi ya msingi inadaiwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema, mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Mdee alitamka maneno dhidi ya  Rais John Magufuli kuwa,  ‘anaongea hovyo, anatakiwa afungwe breki,’ kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kusababisha uvunjifu wa amani.