VIDEO: Lipumba: Hali ya kisiasa nchini kwa sasa ni tete

Muktasari:

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema kwa sasa hali ya kisiasa nchini ni tete, hususan kwa vyama vya upinzani kutokana na kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema kwa sasa hali ya kisiasa nchini ni tete, hususan kwa vyama vya upinzani kutokana na kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara.

Mara baada ya kuingia madarakani, Rais John Magufuli alipiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano ya kisiasa isipokuwa kwa viongozi wa kuchaguliwa (wabunge na madiwani) ambao wanatakiwa wafanye katika maeneo yao.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya vyama au wanasiasa waliojaribu kufanya hivyo, wamekumbana na nguvu ya dola baada ya mikutano yao ama kuzuiwa au kuvunjwai.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili juzi, Profesa Lipumba alisema “kwa vyama vya upinzani hali ni tete na ni ngumu. Tumezoea kuwa kueleza sera, kueneza sera na kuvutia wanachama kujiunga na chama hutegemea mikutano ya hadhara lakini kwa sasa sasa hairuhusiwi,” alisema.

Alisema licha ya hali kuwa hivyo, taratibu na Sheria ya Vyama vya Siasa (namba 5) inaeleza kuhusu uhuru wa kufanya shughuli za kisiasa, kufanya mikutano ya hadhara na maandamano kwa kufuata utaratibu kwa kutoa taarifa kwa ofisa mfawidhi wa polisi.

“Kama polisi wana sababu ya kupinga mkutano huo, watakupa utaratibu na kukueleza ni lini unaweza kufanya mkutano huo. Lakini ukiandika barua polisi, unaambiwa Rais amekataza mikutano ya hadhara,” alidai Lipumba.