VIDEO: Makamba aainisha kinachopunguza mchango wa diaspora

Muktasari:

  • Serikali yajipanga kuhakikisha inaongeza mchango wa diaspora kwenye uchumi wa Taifa.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ameeleza sababu za mchango wa Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) kuwa mdogo, akibainisha namna hadhi maalumu itakavyoongeza mchango wao kwa Taifa.

Makamba amebainisha hayo wiki hii katika mahojiano maalumu Mwananchi Digital.


Makamba azungumzia mchango wa Diaspora, utendaji wa mabalozi nje ya nchi

Amesema utaratibu wa hadhi maalumu watakayopewa raia wa mataifa mengine wenye asili ya Tanzania utawekwa kisheria kwenye mkutano ujao wa Bunge kwa kuzifanyia marekebisho sheria mbili.

Sheria hizo ni ya Uhamiaji, ili kuruhusu vibali vipya ambavyo havina ukomo, na Sheria ya Ardhi, ili kuruhusu umiliki wa ardhi.

Makamba amesema diaspora wana mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa kwa maana ya kuleta fedha nchini na kuwa kiwango wanacholeta kwa sasa kimefikia Dola za Marekani 700 milioni (Sh1.77 trilioni) kwa mwaka.

Hata hivyo, kiwango hicho ni kidogo ukilinganisha na mataifa mengine kama Nigeria ambayo mwaka 2023, diaspora wake walichangia Dola za Marekani 25 bilioni na Kenya ambayo kwa mwaka huo walichangia Dola za Marekani 4.19 bilioni.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (kulia) akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa Mwananchi, Peter Elias Alhamsi Machi 21, 2024. Picha na Michael Matemanga


Changamoto zilizopo

Makamba amesema kuna changamoto mbili kwa diaspora wa Tanzania zinazosababisha wawe na mchango mdogo ukilinganisha na mataifa mengine.

Mosi, amesema Watanzania wamechelewa kutoka nje, nchi nyingine watu walianza kutoka tangu miaka ya 1950 lakini Tanzania ilibaki nyuma, hivyo idadi ya walioko nje ni ndogo na kiwango wanacholeta nchini ni kidogo.

Pili, ni aina ya shughuli ambazo Watanzania wanafanya nje ya nchi, ambazo amesema zinawafanya wapate kiwango kidogo cha mapato, hivyo mchango wao pia kuwa mdogo.

“Kilio cha Watanzania kilikuwa ni sheria kutowaruhusu kumiliki mali kwa sababu wana uraia wa nchi mbili, kutorithisha mali kwa sababu wana uraia wa nchi nyingine, kutofungua akaunti benki na kuwekeza. Kutokana na hilo, Serikali ikaamua ianzishe kitu kinaitwa hadhi maalumu ambayo inajibu kilio cha muda mrefu cha watu wenye asili ya Tanzania na uraia wa nchi nyingine, ili waweze kutoa mchango kwa nchi yao,” amesema na kuongeza:

“Hadhi maalumu inatoa baadhi ya haki, kwa mfano haki ya kumiliki ardhi. Mtanzania mwenye pasipoti ya Canada, Uingereza au ya Marekani, ilimradi ana asili ya Tanzana, sasa ataruhusiwa kumiliki ardhi kama ambavyo Mtanzania ana haki, na atakuwa na uwezo wa kurithisha ardhi hiyo,” amesema.

Amesema kuna vitu vingine vidogo kama vile mtu kuwalipia wazazi wake bima au akitaka kuwekeza, vivutio vitakuwapo.

Makamba amesema mtu mwenye asili ya Tanzania lakini ana uraia wa nchi nyingine, hatalazimika kuwa na viza kwa ajili ya kuja Tanzania kwa kuwa tayari wamemtambua, hivyo ataruhusiwa kuja nchini moja kwa moja bila viza na akija Tanzania anaweza kukaa muda wowote anaotaka.

“Kwa hiyo, kuna vitu vingi ambavyo hadhi maalumu inavitoa ambavyo Watanzania wengi wa nje wanavitaka. Imani yetu ni kwamba hiyo itasaidia Watanzania kuja zaidi kuweka mtaji na kuwekeza,” amesema.


Ulinzi wa diaspora

Makamba amesema Tanzania imeingia mkataba na mataifa mengine ili kuweka taratibu za kuwezesha au kurasimisha ajira ambazo Watanzania wanapata hasa katika nchi za Kiarabu ili ziwe zenye staha na za haki, mapato yao yapatikane na changamoto zilizokuwapo zisiwepo tena.

Amesema Serikali inatoa wito kwa Watanzania waliopo nje ya nchi kujisajili kwenye mfumo (diaspora portal) ili wajulikane walipo na wakipata matatizo iwe rahisi kuwasaidia kokote waliko.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza Watanzania kokote walipo, wazingatie sheria za nchi husika, kwani wasipofanya hivyo Serikali haiwezi kuwasaidia.

Hata hivyo, pale Watanzania wanapoonewa kwa sababu ya Utanzania wao, Serikali itatumia rasilimali zake kuwatetea.

“Yametokea matukio ya namna hiyo, tumeingilia kati. Mimi kama Waziri napiga simu kwa waziri mwenzangu, naisumbua Serikali kwa kuwa kila Mtanzania ana haki ya kulindwa, huo ni wajibu wetu kutimiza,” amesema.


Ufanisi balozi za Tanzania

Waziri Makamba ameeleza kuwa ufanisi wa balozi za Tanzania duniani ni mchanganyiko, zipo zinazofanya vizuri na zinazohitaji kuimarisha utendaji wake.

Amerejea kauli ya Rais Samia, wakati akizindua kamati aliyoiunda, akizungumza kuhusu changamoto anazoziona kwenye balozi.

“Yale maelezo yake pamoja na matokeo ya kamati aliyoiunda kwa ajili ya kutathmini kazi ya wizara tunayapokea na tunayafanyia kazi, tunayachakata na matokeo yake ni kwamba Aprili, kuanzia tarehe 20, tumewaita mabalozi wote 46 na konseli kuu tano duniani, tutakaa sehemu huko Kibaha kwenye shule ya uongozi kwa siku nne kujadili utendaji wa kila ubalozi,” amesema.

“Pamoja na kurejea maelekezo ya jumla aliyoyatoa Rais, katika kipindi hiki cha miezi minne iliyopita, tumekuwa tunafanya uchambuzi wa kina wa kila ubalozi na kila fursa iliyopo ili tuweze kutoa maelekezo, malengo na vipimo mahususi,” amesema.

Waziri Makamba amesisitiza kuwa watakapowaita watawapa KPIs (vipimo vya utendaji) ambazo zimetokana na uchambuzi wa fursa zilizopo, changamoto na mazingira yaliyopo katika kila balozi.

“Tunaona hiyo ni njia bora zaidi kuliko kufanya ya jumla kwa sababu vituo vinatofautiana. Balozi wetu Malawi, huwezi kumpa performance indicators (vipimo vya utendaji) vinavyofanana na vya balozi wetu wa Beijing. Kwa hiyo, kazi ambayo tumeifanya ni kuchambua mazingira mahususi ya kila nchi, kila ubalozi ili tuweze kutoa vipimo tofauti kwa kila balozi,” amesema.


Mafanikio ziara za Rais

Kuhusu ziara za Rais Samia katika mataifa mbalimbali, Makamba amesema zimekuwa na mafanikio ya moja kwa moja na yasiyo ya moja kwa moja.

Amesema mafanikio hayo yametokana na kauli yake, neno lake na ushawishi wake aliposafiri.

Kwa mfano, amesema mwaka jana, Rais alienda Marakesh, Morocco kwenye Jukwaa la Uwekezaji Afrika ambalo lilikusanya watu wenye fedha duniani na nchi zikapeleka miradi yake. Amesema Rais Samia alienda na miradi ikiwemo ya Bandari ya Mangapwani, Zanzibar, reli ya Ziwa Nyasa – Mbambabay mpaka Mtwara na mradi wa SGR (reli ya kisasa).

Waziri Mkamba amesisitiza kiwango cha uwekezaji kilichoongezeka kufikia Dola 5.6 bilioni mwaka jana (Sh14.22 trilioni) kimetokana na safari zake, mikutano aliyofanya alikoenda, na wawekezaji aliokutana nao.

Amesema unapofika kiwango hicho cha uwekezaji (Dola 5.6 bilioni) kutoka Dola 1 bilioni, ni kwamba ajira zimeongezeka, mtaji (fedha za kigeni) umeongezeka, mapato ya Serikali yameongezeka, teknolojia mpya imeingia na utoaji wa huduma za jamii umeongezeka.

“Tukienda nje watu wanadhani tunaenda kupumzika, lakini ratiba ambayo Rais anakuwa nayo, ni ambayo hata kijana wa miaka 20 atatoa ulimi nje… sisi tuliopo tunaona, kwa kweli ziara zake zina manufaa makubwa,” amesema.

Makamba amesema kutokana na fursa zilizopo huko duniani, Tanzania inaweza kufikia lengo la Dola 2 bilioni (Sh5.08 trilioni) kwa mwaka, kwa sasa imefikisha zaidi ya Dola 1 bilioni.

Amesema kufikisha Dola 10 bilioni ifikapo mwaka 2025 haitakuwa ajabu.