VIDEO: Makamba ataja mambo manne kumpata rais
Muktasari:
Mbunge mteule wa Bumbuli (CCM), January Makamba amesema ikiwa zimebaki siku nane Watanzania kupiga kura kuchagua rais, wabunge na madiwani kuna mambo manne ya kuzingatia ili kumchagua kiongozi mkuu wa nchi.
Korogwe: Mbunge mteule wa Bumbuli (CCM), January Makamba amesema ikiwa zimebaki siku nane Watanzania kupiga kura kuchagua rais, wabunge na madiwani kuna mambo manne ya kuzingatia ili kumchagua kiongozi mkuu wa nchi.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni ubora wa sera, ilani ya uchaguzi, chama na mgombea.
Alieleza hayo leo Jumanne Oktoba 20, 2020 katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa CCM, John Magufuli uliofanyika mjini Korogwe Mkoa wa Tanga.
Amesema wapiga kura lazima waangalie rekodi na historia ya vyama katika kutekeleza ahadi zake nakuongeza kuwa historia ya CCM ni kuaminiwa katika uongozi wa nchi, kuongoza nchi kwa utulivu na usalama pamoja na ustawi.
Amedai kati ya vyama vyote vilivyosajiliwa hakuna hata kimoja chenye sifa na sura ya kitaifa kama CCM huku akiwataka wananchi kuangalia uimara wa mgombea na chama.
"Hata ukimsikia Rais wetu Magufuli anavyohutubia kwenye mikutano yake ya kampeni wala hatukani mtu, hamsemi mtu wala hamlalamikii mtu bali anazungumza mambo yanayogusa mahitaji ya wananchi na hiyo ni sifa nyingine aliyonayo mgombea wetu,” amesema Makamba