VIDEO: Manusura ajali ya bodaboda afunga ndoa wodini

Tuesday September 21 2021
By Sharon Sauwa

Dodoma. Ajali ya pikipiki iliyotokea katika maungano ya reli na barabara eneo la Zuzu jijini hapa haukukatisha furaha na mipango ya Augustino Makule (29) kufunga ndoa na kipenzi chake, Rose Kimaro (29).

Baada ya maandalizi yaliyofanyika kwa muda mrefu kuwashirikisha ndugu, jamaa na marafiki, Augustino alipata ajali na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Septemba 14 alikolazwa katika katika wodi namba mbili.

Ingawa ajali hiyo imemuacha akikatwa mguu na kupoteza vidole vitatu vya mguu wa kushoto, wawili hao waliibua shangwe wodini humo baada ya kufunga ndoa Takatifu ambayo awali ilipangwa kufungwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Nkhungu jijini hapa. Siku ya ndoa hiyo ilitarajiwa kuwa Septemba 18, hata hivyo, ilifungwa siku hiyohiyo.

Akisimulia kuhusu ndoa hiyo iliyovuta hisia za wagonjwa wa wodi hiyo, muuguzi wa wodi ya magonjwa ya mifupa, Winfrida Elias alisema ilifungwa saa 9:00 alasiri ambapo Augustino alikaa katika kiti cha wagonjwa (wheelchair) kilichonunuliwa na ndugu na marafiki kwa ajili hiyo na ziliimbwa nyimbo za ibada tu na ikamalizika muda wa kuona wagonjwa, saa 10 jioni.

Bwana harusi alipata ajali siku tatu kabla ya ndoa, ili kuifanikisha hospitalini hapo, nesi alisema waliondoa vitanda viwili katika wodi hiyo ilikupata nafasi ya kupamba bila kuleta usumbufu kwa wagonjwa wengine. Walifanya hivyo baada ya ndugu na mchungaji kuomba kwa uongozi wa hospitali.

“Tuliwaandalia mazingira ya kuwawezesha kupamba na kukaa wodini bila kuwabughudhi wengine. Wagonjwa waliokuwepo walishiriki katika harusi hiyo ingawa hatukuruhusu wapigwe picha.Kila mmoja alifurahia,” alisema Winfrida.

Advertisement

Takriban ndugu 30 walishiriki ibada ya ndoa hiyo iliyofanyika kwa saa moja tu kisha kuwaruhusu wanaofika kuwaona wagonjwa wengine kupata nafasi. Baada ya mchungaji kukamilisha ibada, keki ilikatwa na kuliwa.

Ajali ilivyojitokea

Jumanne jioni wiki iliyopita Makule akiwa na rafiki yake aliyekuja kutoka Mwanza kuhudhuria harusi yake walitoka kwenda kuangalia mechi ya Chelsea ilikuwa ikicheza na Zenit St. Petersburg kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Rafiki yangu alikuja kunisaidia maandalizi ya sherehe lakini akaniambia ngoja nikaangalie mpira, yeye ni mpenzi wa Chelsea. Nikamwambia kuna sehemu wanaonyesha ngoja niite bodaboda,” alisema.

Kwa kuwa dereva alikuwa mbali waliamua kutembea kwa miguu ila wakati wakienda aliona mama anauza maandazi hivyo akanunua na kumuomba rafiki yake amsubiri ayapeleka nyumbani. Ili awahi, alichukua bodaboda lakini walipofika kwenye maungano ya Reli ya Kati na barabara eneo la Zuzu walipata ajali kwa kuigonga treni.

“Nadhani wale jamaa (reli) walifunga sehemu ya kuingia ila wakaacha wazi ya kutokea hivyo sisi tukapitiliza ndio tukaivaa treni, wengine walirushwa mimi ndio likaniburuza kidogo,” alisema.

Makule ambaye ni mtaalam wa ardhi (quantity surveyor) alisema alikaa kwa saa 24 bila kujitambua hospitalini hapo. Hata hivyo, alisema anamshukuru Mungu kufunga ndoa na mke wake waliyeishi kinyumba kwa miaka minne sasa.

Ndoa hospitalini

“Mungu aliipenda hii kitu na alitushindania na ametushindia sana. Mchungaji hakuwa na taarifa, alipozipata alikuja hospitalini akaomba kuniona. Tulipokutana akaniuliza kama nipo tayari kufungia ndoa hospitalini hapon ami nikakubali,” alisema.

Awali ndoa hiyo ilipangwa ifanyike katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Nkhungu na sherehe katika Hoteli ya St Gasper.

“Tulishalipa advance (malipo ya awali), kila kitu kilikuwa tayari. Na siku niliyopata ajali nilikuwa narusha ‘pre wedding photo’. Kwa hiyo ilikuwa kama surprise watu walikuwa wanahoji mbona huyu jamaa anatupostia halafu wanasema amepata ajali,” alisema.

Kwenye sherehe ya harusi yao, alisema walipanga ihudhuriwe na watu 100 tu lakini wodini hapo wakaruhusiwa wachache kutokana na mazingira kutoruhusu.

Bibi harusi Rose alisema mumewe na shemeji yake walimuaga saa moja usiku kuwa wanakwenda kuangalia mpira lakini ilipofika saa tatu akapata taarifa kuwa mumewe amepata ajali.

Hata hivyo, alipomuona alimsisitiza kufuatilia kwa mchungaji ili wafunge ndoa kama ilivyopangwa. “Nikawatafuta wazazi tukaenda nao kanisani mchungaji akakubali,” alisema.

Rafiki wa bwana harusi, Baraka Malecela alisema kwa jinsi ajali ilivyotokea, hakuna aliyefikiri kuwa ndoa hiyo ingeweza kufungwa lakini juhudi zilizofanywa zimefanikisha ifungwe wodini.

“Mtu wa kwanza kutupa matumaini na kufufua hali tuliyokuwa nayo ni Augustino mwenyewe kwa kweli alitu-suprise sana. Yeye ndiye alikuwa mtu wa kwanza kusema ndoa ipo kama kawaida Jumamosi (Septemba 18) na itafungwa hapa hapa hospitalini,” alisema Malecela.

Baada ya mgonjwa kuonyesha utayari wake wa kufunga ndoa bila kujali hali aliyonayo, Malecela alisema ilikuwa rahisi kwao kufuata utaratibu unaokubalika hospitalini hapo ili kutimiza malengo.

Advertisement