Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Mwonekano mpya wa Muhimbili ya Profesa Janabi

Muktasari:

  • Licha ya kuwa na wadhifa mkubwa, lakini Watanzania wengi wanamfahamu Profesa Mohammed Janabi kutokana na mafunzo na maonyo yake kuhusu afya. Lakini, kwa sasa Profesa Janabi anakuja kuandika historia ya kuifanya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwa....

Dar es Salaam. Miaka minne ijayo, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) nchini Tanzania itakua na mwonekano mpya, baada ya kuanza rasmi upembuzi yakinifu wa mwonekano utakavyokuwa wakishirikiana na Serikali ya Korea.

Ujenzi huo utahusisha ubomoaji wa wodi zote kubwa ikiwemo Sewahaji, Kibasila na Mwaisela ili kujenga majengo mengine mapya ya kisasa.

Majengo ya hospitali hiyo yalijengwa miaka 104 iliyopita.

Hayo yamesemwa juzi Jumanne, Februari 20, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohammed Janabi katika mahojiano maalumu na Mwananchi Digital.

“Tumeanza kufanya upembuzi yakinifu, tutaanza kuibomoa Muhimbili kwa awamu ili kuja na hospitali kubwa na ya kisasa zaidi, tukishirikiana na wenzetu wa Korea,” amesema.

Amesema upembuzi huo yakinifu umeanza mwezi huu kwa wataalamu wa ndani na Korea kushirikiana pamoja na kwamba awamu ya kwanza imeshaandaliwa.

Mwonekano mpya wa Muhimbili ya Profesa Janabi

“Awamu ya kwanza imeshakamilika na  tutaanza kubomoa huu upande ambao kuna chuo cha uuguzi na hosteli. Tutaanza ujenzi eneo hilo kwanza, ili tuweze kuhamisha taratibu wagonjwa waliokuwa Mwaisela na Kibasila kuja kuhamia kwenye jengo jipya.

“Mungu akipenda kwa muda mfupi wa ndani ya miaka minne, tutakuwa na hospitali yetu mpya humuhumu ndani ikiwa imekamilika na ndiyo maana tunajenga kwa awamu,” amesema Profesa Janabi.

Maboresho hayo yanakuja miaka 104 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo miaka ya 1910 hadi 1920 ikijulikana kama Hospitali ya Sewahaji.

Profesa Janabi amesema mwaka 1956 jina lilibadilishwa na kuwa Hospitali ya Princess Margareth.

“Wakati inaanzishwa nilikuwa sijazaliwa na wengi tulikuwa hatujazaliwa, mara baada ya Uhuru mwaka 1961 iliitwa Hospitali ya Muhimbili hadi 1976 ilipobadilishwa na kuwa Kituo cha Tiba cha Muhimbili.

“Hospitali ya Taifa Muhimbili yaani MNH ilianzishwa na Sheria ya Bunge ya MNH namba 5 ya mwaka 2000 kwa kutenganisha Kituo cha Tiba cha Muhimbili (MMC) na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUCHS) sasa Chuo Kikuu cha Muhimbili, Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS). Utengano uliofanyika Novemba 2004,” amesema.


Uongozi Muhimbili

Wakati kukiwa na mabadiliko makubwa Muhimbili kwa sasa, Profesa Janabi amesema alianza kuiongoza hospitali hiyo Oktoba 2, 2022 na kabla hajaingia alikuta mambo mengi yameshaanza.

Amesema baada ya kuchukua kijiti aliendeleza yale yaliyokuwepo na kuongeza baadhi ambayo yalihitajika kulingana na mabadiliko ya nyakati.

“Tumeweza kuzidisha imani ya wananchi kuja katika hospitali hii ya Taifa, ambayo ndiyo kubwa kuliko zote katika nchi zote kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, ina vitanda 2,200.”

“Pia ni kubwa kwa kuwa ukitaka wataalamu wa aina yoyote, Muhimbili ndiyo yenye wataalamu zaidi ya asilimia 82 ya wale wanaohitajika, katika magonjwa yote ukiacha yale ya moyo ambayo yako JKCI (Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete),” amesema Profesa Janabi.

Amesema kutokana uwekezaji mkubwa uliofanywa katika miaka mitatu hadi minne kwenye afya ya msingi, mabadiliko ya idadi ya wagonjwa pia yamekuwa makubwa.

“Kama huko chini kuna uwekezaji lazima sisi tuanze kubuni vitu ambavyo haviwezi kufanywa huko chini, sasa hivi tunapandikiza figo, uloto, vifaa vya kusikilizia, tumeingia kwenye upasuaji wa kurekebisha maumbile.”

“Pia tumefanya operesheni kubwa kwa mwalimu mmoja kutoka mikoa ya Kaskazini ambaye alipofuka sababu ya uvimbe kichwani, na tulipoutoa uvimbe kupitia pua, nusu saa tu aliweza kuona tena,” amesema.

Amesema kumekuwepo na huduma mbalimbali mpya za wataalamu bingwa kuungana pamoja ikiwemo mabingwa wa upasuaji wa kifua, moyo, mapafu na mfumo wa upumuaji kutoa matibabu.

Amesema hivi karibuni wamerekebisha watoto zaidi ya 21 waliokuwa na jinsia tata, pamoja na kuanza kufanya  upandikizaji mpya wa nywele kwa watu wenye vipara.

“Nikijaribu kutizama nyuma huu mwaka mmoja, mbali ya upasuaji, usafi wa hospitali yetu umeimarika, tumejaribu kuondoa kumjua daktari kwa ajili yakupata huduma ambapo sasa mfumo upo na ndio utakaomuhudumia kila mmoja,” amesema.

Kuhusu upasuaji

Akizungumzia kuhusu upasuaji, Profesa Janabi amesema Muhimbili ndiyo yenye wataalamu bobezi wengi kuliko hospitali nyingine yoyote.

“Iwe za Serikali au binafsi na kwa sababu kuna fani tofauti tunapanga kwa kuangalia kutokana na magonjwa 10 yanayoongoza hapa,” amefafanua.

Ametaja changamoto ya ugonjwa wa figo hivi sasa ni kubwa sana, ambapo wagonjwa wanaosafishwa figo katika kampasi ya Upanga ni 110 hadi 120 kila siku na kwa kampasi ya Mloganzila ni karibu 30 kwa siku, hivyo hicho ni kipaumbele.

Amesema huduma ya kupandikiza uloto ni tatizo kubwa lililopo hasa kwa watoto, tatizo la usikivu pia watoto wengi wanatibiwa huku akitolea mfano mtoto wa balozi mmojawapo Tanzania mwenye umri wa miaka minne ambaye alisikia kwa mara ya kwanza hivi karibuni, baada ya Muhimbili kumfanyia upasuaji.

“Kwa hiyo kwanza tunapopanga masuala ya upasuaji tunaangalia tatizo tulilonalo kwa ukubwa hapa ndani. La pili tunaloangalia ni nchi tunazoshirikiana nazo, kwa mfano kupandikiza nywele kuna wataalamu kutoka Marekani ambao tunashirikiana nao, kwa hiyo wanajenga uwezo wa ndani.”

“Tutafanya mara ya kwanza, mara ya pili, mara ya tatu na mbeleni tutaendelea wenyewe na siyo kitu ambacho hakiwezekani, inawezekana,” amesema na kuongeza;

“Nimekaa miaka minane kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tulifanya hivyo na ndiyo iliyoifikisha taasisi hiyo hapo, kwa kutumia mtindo huo. Mtaalamu anapokuja anafundisha wengi ambao wako kwenye mazingira yetu, kwa hiyo ile hali ya kujiamini ya wataalamu inakuwa kubwa zaidi wanapofanya kwenye eneo la nyumbani,” amesema.

Profesa Janabi amesema hata wanapoanzisha huduma mpya za upasuaji ikiwemo wa maumbile, puto wanatoa kipaumbele kwa yale matatizo yaliyopo kwenye jamii. “Hatuwezi kufanya upasuaji kwenye eneo ambalo halina mgonjwa, kwa hiyo uhitaji ndio unaotuelekeza nini cha kufanya kwa wakati gani.”


Upandikizaji mimba

Licha ya huduma hii kusubiriwa kwa muda mrefu, Profesa Janabi amesema Muhimbili inatarajia kuanza rasmi kutoa huduma za awali ya upandikizaji mimba ifikapo Mei 2024.

“Kununua vifaa ni kitu kimoja na kufunga ni kitu kingine, hii ni kwa kuwa wakati unafanya utaratibu wa kununua vitu, ni lazima wakati huo huo unaanza na utaratibu wa kufundisha watu kwa sababu huwezi kuleta vifaa halafu hakuna wataalamu wanaoweza kuvitumia,” amesema.

Amesema uletaji vifaa ulichukua muda wa miaka mitatu, walikuwa pia wanajenga uwezo wa wataalamu wa ndani.

“Tulipeleka watu kwenda kusoma Marekani, India na kuchukua wengine kwenye hospitali binafsi ambazo zilikuwa zinafanya huduma kama hii, lakini pia tutakuwa na hawa wenzetu waliotuuzia hivi vifaa katika siku za mwanzo za utoaji huduma,” amesema.

Katika kukamilisha huduma hiyo, Profesa Janabi amesema tayari wameshaweka vifaa kwenye majengo kwa asilimia 100 vilivyofungwa ndani ya miezi minne, “Si jambo jepesi. Kutakuwa na uwezekano hata wa kutunza mayai ya wanawake hasa wale wenye umri mdogo wasiotaka kuzaa mapema ili wakati watakapokuwa na uhitaji waweze kuja kupandikizwa mayai yao na kupata watoto.”

Mbali ya kuwapa nafasi akina dada kujifungua katika muda wanaotaka, amesema itasaidia zaidi kuweka ndani fedha za kigeni kupitia utalii wa tiba kwa kuwaleta watu wengi kutoka mataifa mbalimbali, kwa kuwa itakuwa huduma ya viwango vya juu kabisa duniani.

Umuhimu wa bima kwa wote

Miongoni mwa changamoto nyingi alizozitaja Profesa Janabi zinazotokea na kuleta changamoto zinasababishwa na wagonjwa wengi kutokuwa na bima, hivyo kushindwa kulipia huduma baada ya matibabu na kama mgonjwa akifariki.

Amesema hiyo husababisha hospitali kutoa msamaha wa zaidi ya Sh1.3 bilioni kila mwezi.

“Kila mwezi Muhimbili inatoa msamaha wa Sh1.3 bilioni hadi Sh1.5 bilioni. Huyu mtu ataingia humu ndani, ataonwa na daktari, kama upasuaji atafanyiwa, atakaa chumba cha uangalizi maalumu (ICU), atapewa dawa na siku ya kuondoka atapewa dawa za mwezi mzima.”

“Atapewa pia chakula, ambapo bili yetu ya chakula sisi kwa mwezi ni mpaka Sh200 milioni kwa wagonjwa waliolazwa, bila kulipa hata senti tano, ambayo ipo ndani ya hiyo Sh1.5 bilioni,” amefafanua na kuongeza;

“Lakini hii tunasema siyo bure kwa sababu Serikali ndiyo inayolipia, hapo kuna dawa zimenunuliwa, kuna vifaa vimetumika sasa tunaposema wananchi wapate unafuu, sijui ni unafuu gani kwa sababu kama kwa mwaka tunaweza kutoa msamaha wa Sh18 bilioni, ina maana Serikali inafidia hapo,” amesema.

Profesa Janabi amesema Serikali haiwezi kumlipia kila mtu. Ndiyo maana imekuja na muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote iliyopita bungeni na kupitishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa sheria.

“Hii inakuja ili tuweze kuchangia katika matibabu na mwananchi awajibike kwa sababu hapimi afya kila mwaka, hafanyi mazoezi, anakula chakula kisicho sahihi, anakunywa pombe kupitiliza, baadhi wanatumia dawa za kulevya, wanavuta sigara halafu wanategemea afya zao ziwe sawasawa, hapana, ni lazima wawajibike,” amesema.

Amehoji mwananchi lazima ajiulize amechukua jukumu gani kukinga afya yake, hilo ni jambo muhimu.

“Vinginevyo tutaishia kuilaumu Serikali, lakini mimi nasema Serikali ni mimi na wewe,  pale moyo unapokuwa mkubwa kwa kunywa pombe kupita kiasi, mapafu yanapopata saratani, atakayeumia zaidi ni wewe.

“Sasa mimi ninashauri, kila mmoja wetu ajaribu kuishi maisha yale yanayoshauriwa na wataalamu na wawe na utaratibu wa kuchunguza afya kila mara, wengi hatufanyi, tuache hofu kwa sababu hofu haisaidii kukinga ugonjwa,” amesema Profesa Janabi.

Kiwango cha ubora wa wanafunzi Muhas

Licha ya kuwepo kwa taarifa za kushuka kwa kiwango cha Chuo cha Afya Muhimbili Muhas, Profesa Janabi amesema anaridhika na ubora akisisitiza hatua zinapaswa kuchukuliwa.

“Mimi ni mwalimu chuo cha Muhas kwa miaka mingi na ninaendelea kufundisha, kuhusu ubora ninaridhika sana kwa sababu wanaozalishwa ndio wanaoendesha sekta ya afya.”

“Kumekuwa na maboresho kwa sababu walimu nao wanazidi kuongezeka. Chuo chetu mwaka jana kilikuwa namba tano kwa Afrika katika vyuo vikuu, mwaka huu nasikia tumetetereka kidogo lakini ni vitu tunavyoweza kuvifanyia kazi,” amesema.

Maegesho Muhimbili

Malipo ya maegesho ya magari Muhimbili ni suala linalozungumzwa sana kwa sasa tangu mfumo huo uanzishwe.

Hata hivyo Profesa Janabi amesema walianzisha mfumo huo si kwa ajili ya kupata mapato, bali ilitokana na utafiti walioufanya.

“Tulianzisha maegesho kutokana na utafiti ambao tuliufanya mara baada ya mimi kuingia hapa. Tulibaini  Muhimbili yaliingia magari 5,000 kwa siku, kila kutwa kukikuwa na magari 1,000 humu ndani yamepaki mpaka jioni ilhali maegesho yapo ya magari 240.”

“Tukagundua watu wanapaki magari hapa, wanakwenda kupanda mwendokasi wanakwenda mjini na kutuachia huo mzigo kwa sababu humu ndani kuna uhakika wa usalama,” amesema.

Hata hivyo changamoto iliyoibuka ni uwepo wa malalamiko ya watu kutozwa fedha za maegesho wakati utoaji huduma unachukua muda mrefu, hivyo kusababisha gharama kubwa za maegesho.

“Kuna utaratibu tumeuweka, kuna wagonjwa wanaokuja kwa ajili ya huduma za muda mrefu wakiwemo wa kusafisha figo, wale wanavibali kukaa pale bila kulipia na wanajua utaratibu wao na wana viongozi wao,” amesema.