VIDEO-Polisi yachunguza chanzo cha mauaji Padre Mbeya

Polisi yachunguza chanzo cha mauaji Padre Mbeya

Muktasari:

Padre huyo aliaga kanisani kwake kwenda kufanya mazoezi Juni 10, ambapo Juni 11 mwili wake ulikutwa kwenye mto Meta jijini Mbeya akiwa amechinjwa na viungo vyake kutengenishwa na kuwekwa kwenye blanketi.

Mbeya. Jeshi la Polisi mkonai Mbeya limethibitisha kutokea mauaji ya Padre wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya wa Shiriki wa Wasionari wa Afrika (White Father), Michael Samson huku likieleza kuendelea na uchunguzi kujua chanzo cha kifo hicho.

Padre Samson anadaiwa kuuawa na watu wasiojulikana kwa kukatwa viungo na kutengenishwa kisha kutupwa katika mto Meta maeneo ya Sabasaba jijini hapo.

Katika taarifa iliyotolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Mbeya, Mhashamu Gervas Nyaisonga jana Jumamosi ilieleza kuwa Padre Samson alitoweka Juni 10 katika kituo cha Vijana kanisa Katoliki Mbeya saa 12 jioni.

Taarifa hiyo ilieza kuwa baadaye mwili wa padre huyo uliokotwa maeneo ya Sabasaba jijini humo Juni 11 majita ya saa 4 asubuhi.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya (RPC), Ulrich Matei amesema wanaendelea kufanya uchunguzi kunaini chanzo cha mauaji hayo, kwani marehemu alikuwa raia wa Malawi na kuwaomba wananchi kutoa taarifa ili kukamatwa kwa wahusika.

Amesema kwa uchunguzi wa awali wamebaini ni mauaji ya makusudi na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kutumia njia za kisayansi ili kumbaini aliyetekeleza mauaji hayo.

"Tumechukua maelezo kwa watumishi wenzake kujua kama huyo marehemu alikuwa na mgogoro popote lakini kila mmoja anasema hapana, huyu ni raia wa Malawi na alikuwa na mwaka mmoja amehamishiwa hapa, tutafuatilia hadi alipotoka tunaamini tutafanikiwa, niwaombe wananchi kutojichukulia sheria mkononi" amesema Matei.