VIDEO: Profesa Lipumba ashtushwa namba kuandikwa daftarini

VIDEO: Profesa Lipumba ashtushwa namba kuandikwa daftarini

Muktasari:

Mgombea urais kwa tiketi ya CUF,  Profesa Ibrahim Lipumba ameshtushwa na utaratibu wa kuandika namba ya kitambulisho cha mpigakura katika karatasi ya kura unaofanywa vituoni .

Dar es Salaam. Mgombea urais kwa tiketi ya CUF,  Profesa Ibrahim Lipumba ameshtushwa na utaratibu wa kuandika namba ya kitambulisho cha mpigakura katika karatasi ya kura unaofanywa vituoni .

Baada ya kupiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Mtakuja jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba alionyesha kushangazwa na utaratibu huo, akisema unamaanisha hakuna siri katika kupiga kura.

Mara baada ya mpigakura kuingia kituoni, hutakiwa kukabidhi kitambulisho chake kwa marakani ambao mmoja wao hutafuta jina katika Dakftari la Kudumu la Wapigakura na anapoliona, hutaja namba iliyo sehemu hiyo na karani mwingine kuiandika katika moja ya karatasi za kupigia kura na ndipo nyaraka hizo hizo tatu hukabidhiwa kwa mpigakura.

Lakini Profesa Lipumba anaona kitendo hicho kinawezesha kufahamu mpigakura amewapigia wagombea gani.

“Kwa hiyo si kura ya siri kwa sababu ile namba ya kitambulisho cha kupigia kura imeandikwa katika ballot paper,” alisema.

“Kwa hiyo mtu akiisoma ile namba ya kupigia kura, akienda tu kwenye tovuti ya Tume—hata wewe (mwandishi) ukienda-- ukaiweka ile namba, unajua mpigakura ni nani.

“Kwa hiyo kila kura itakayopigwa itajulikana ni nani kampigia kura.”

Haikuwezekana mara moja kuwapata NEC kuzungumzia utaratibu huo.

Kuhusu matarajio yake katika uchaguzi, Profesa Lipumba, ambaye alifika kituoni saa 5:30 kupiga kura,  amesema ana uhakika wa kushinda.

"Nimejiandaa vizuri, pamoja na changamoto zote, nchi bado ni yetu tusiwe na tatizo. Tusubiri matokeo tusiingie katika hali ya uvunjifu wa amani, tuwe wavumilivu ujenzi wa demokrasia ni mchakato ambao unachukua muda mrefu," amesema Lipumba.

Profesa Lipumba amesema kuna taarifa za mawakala wa vyama vya upinzani kuzuiliwa kuingia ndani katika vituo vya kupigia kura jambo ambalo amelitaja kuwa halitoi ishara ya hali nzuri.

Ametoa wito kwa wananchi kufuata utaratibu sanjari na wasimamizi watende haki, na kama bado kuna mawakala wamezuiwa waruhusiwe ili kazi ifanyike kwa amani.