VIDEO: Rais Mnagangwa aipongeza Tanzania
Muktasari:
Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnagangwa amesema nchi hiyo inaitazama Tanzania kama baba na mama wa uhuru.
Dar es Salaam. Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnagangwa amesema nchi hiyo inaitazama Tanzania kama baba na mama wa uhuru.
Ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba 5, 2020 wakati akizungumza katika hafla ya kuapishwa kwa Rais wa Tanzania, John Magufuli iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
“Rais wa kwanza wa Tanzania hayati Julius Kambarage Nyerere sisi tukiwa Zimbabwe tunamuangalia kama mzalendo kabisa na tunapokuja hapa tunamkumbuka yeye.”
“Nchi nyingi za kusini mwa Afrika pia ikiwemo Afrika Kusini, Zimbabwe, Angola, Namibia, Msumbiji zote zilikuwa hapa na mlitutunza sana, Tanzania imekuwa mwamba wa umajumui wa Afrika katika ukanda wetu na sisi tunajihidi sana kuifuata njia ya waasisi wetu,” amesema.
Ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Magufuli kwa kutembelea nchi yake pamoja na kuwapatia msaada wa mahindi wakati Zimbabwe ilipokabiliwa na ukame shukrani ambazo pia alizielekeza kwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.
“Hawa ndiyo viongozi wazalendo katika ukanda wetu,” amesema Munagangwa.
Amemshukuru pia Rais Magufuli juu ya uamuzi alioufanya alipokuwa Mwenyekiti wa nchi za Jumuiya za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kutangaza Oktoba 25 kila mwaka kuwa ni siku maalumu ya kupinga vikwazo katika nchi yao.
“Ni miaka kumi imepita sasa tukiwa na vikwazo, hatupo tayari kuacha nia yetu ya kurejesha ardhi yetu, Tanzania ndiyo imeongoza, imeonyesha njia katika ukanda wa SADC kuwa vikwazo hivi ni lazima viondoke,” amesema.