VIDEO: Rais Samia kusimama kidete mageuzi ya kiuchumi

Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza katika hafla ya kukabidhi gawio kwa Serikali kutoka kwenye mashirika ya umma na binafsi ambayo Serikali ina hisa zake leo Juni 11, 2024 Ikulu ya Dar es Salaam. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Rais Samia  amepokea gawio la Sh637 bilioni, asema hajali kelele zinazopigwa akimtaka Msajili wa Hazina kusimama imara kusimamia mashirika ya umma

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema ataendelea kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu ajenda ya mabadiliko katika mashirika ya umma.

Amesema kamwe hatayumbishwa na maneno yanayolenga kumtoa kwenye reli.

Katika kutekeleza ajenda hiyo, amemwelekeza Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu kusimama imara kuhakikisha mageuzi hayo yanafanikiwa na kuleta tija kiuchumi.

Rais Samia amesema hayo leo Jumanne Juni 11, 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam alipopokea gawio na michango kutoka mashirika na taasisi 10 za umma.

Amesema Tanzania haina budi kufanya mageuzi ya kiuchumi na mchakato wa kufanya mageuzi hayo ni lazima uhusishe mashirika na taasisi za umma.

Rais Samia ametoa mfano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ambayo imetoa gawio la Sh153.9 bilioni akisema mafanikio hayo ni matokeo ya uwekezaji uliofanyika bandarini ambako kuna wawekezaji wawili.

“Pale TPA mwaka jana kiwango hakikuwa hiki, lakini kwa mageuzi makubwa yaliyofanyika bandarini mwakani tunatarajia makubwa zaidi,” amesema.

“Pale bandarini kuna watu wawili, hivyo tunatarajia makubwa. Wale waliopiga kelele mama kauza bandari, mara kauza bahari mauzo yale faida yake ni hii leo, huu ni mwanzo tunatarajia kupata makubwa zaidi kwa bandari zote,” amesema.

Rais Samia pia, ameonyesha kutoridhishwa na utendaji wa mashirika yanayomilikiwa na Serikali, akimtaka Msajili wa Hazina kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kunakuwa na matokeo chanya.

“Mchechu fanya kazi yako najua utalaumiwa lakini hiyo ndiyo kazi niliyokupa simama ifanye mimi kazi niliyopewa na Watanzania nimesimama naifanya na mnashuhudia matusi ninayotukanwa mpuuzi, hana maana, huyu bibi, yaani mambo tele lakini najigeuza chura,” amesema.

 “Kelele nyingi zinapigwa, wakiona kimya wanaona wanitukane kama nitajibu, sijibu. Ninachotaka ni mageuzi ya kiuchumi katika nchi hii sasa kwenye hayo mageuzi kuna watakaoumia.

“Anayetaka kunikera mimi anikanyagie uchumi wangu, katika mageuzi haya tutawakanyaga wengi wale ambao hawataki kwenda mbele na ndiyo hao watakaopiga kelele,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema hatakuwa na uvumilivu kwa mashirika ya Serikali ambayo yamebweteka yakisubiri msaada kutoka serikalini.

Rais Samia atangaza vita mageuzi ya kiuchumi

Ameyataka mashirika hayo yakajifunze kutoka kwenye mashirika ambayo Serikali imeingia ubia na sekta binafsi.

“Kampuni zilizotoa gawio ni zile ambazo Serikali ina hisa chache kwa maana hisa nyingi ni za sekta binafsi, zile za Serikali hazipo hapa lakini sera ni zilezile ila kampuni zetu zimebweteka. Sekta binafsi wanahangaika kwa kutumia mbinu zote za biashara ili waweze kupata faida, hapa kuna somo kwa mashirika yetu,” amesema.

“Lengo kwenye gawio ni asilimia 11 lakini tupo asilimia tatu ambayo tulikuwa nayo mwaka jana, ni imani yangu kuwa mwakani tutasogea. Tutasogea endapo mashirika 159 ambayo hayakutoa gawio mwaka huu nayo yatajituma kufanya kazi yaweze kuchangia Serikali,” amesema.