Mchango wa wakulima wadogo katika mageuzi ya kiuchumi

Picha inaonyesha wanakijiji wadogo wakiwajibika shambani. Wakulima hawa ni muhimu katika maendeleo ya sekta ya kilimo. Picha na maktaba
Muktasari:
Jitihada zinazofanyika hivi sasa kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa mfano, katika nchi jirani kama Afrika ya Kusini, ni kutengeneza zaidi nafasi za ajira, badala ya kuelekeza nguvu zaidi kwenye kilimo cha mashamba makubwa.
SIRI kuu ya mafanikio katika nchi zinazoendelea ni kilimo.
Hata hivyo, ni dhahiri kwamba kilimo hakiwezi kuleta mafanikio yakinifu bila kuwapo kwa viwanda. Lakini viwanda hivyo havina budi kuwa ni vile vya kusindika na kuchakata mazao ya kilimo.
Kilimo cha biashara ni mujarabu zaidi, lakini hakuna budi kufanyika kwa mipangilio ambayo haitaathiri wakulima wadogo.
Kilimo hicho kisifanyike na kusababisha mamilioni ya wakulima wadogo wakose ardhi ambayo wanaitumia kwa ajili ya shughuli za kilimo cha jembe la mkono.
Suala la mapinduzi ya kilimo, lisitazamwe katika kuongeza uzalishaji wa mazao tu, bali litazamwe katika kutengeneza nafasi nyingi zaidi za ajira.
Jitihada zinazofanyika hivi sasa kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa mfano, katika nchi jirani kama Afrika ya Kusini, ni kutengeneza zaidi nafasi za ajira, badala ya kuelekeza nguvu zaidi kwenye kilimo cha mashamba makubwa.
Kwa mtazamo wangu, kilimo cha mashamba makubwa, kitaongeza uzalishaji kwa baadhi ya mazao, lakini kutakuwapo kwa ukosefu mkubwa wa ajira nchini.
Hivyo basi, kilimo kinahitaji kuendeshwa kwa tahadhari na umakini mkubwa.
Inaelezwa kwamba asilimia 80 ya Watanzania wote wanaishi vijijini. Kati ya hao, wakulima wadogo wanakadiriwa kufikia milioni 20.
Idadi ya mashamba madogo inakadiriwa kuwa si chini ya milioni 4. Nguvu kazi yote nchini inakadiriwa kufikia watu milioni 24 (makadirio ya 2011).
Mageuzi ya msingi ya kiuchumi nchini, hayawezi kufanikiwa ipasavyo iwapo kundi kubwa la wakulima wadogo litapuuzwa au kuachwa pembeni.
Kundi hili lisipuuzwe kama vile halipo au halina umuhimu, bali kundi hilo linapaswa kutazamwa kwa umakini.
Ili kufikia malengo msisitizo usiwekwe tu katika mashamba makubwa pekee ambayo kwa kawaida yanahusisha wakulima wachache.
Moja ya malengo muhimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ni kuitoa Tanzania katika kundi la nchi masikini zaidi duniani na kujenga uwezo zaidi wa kiuchumi utakaoifanya iwe miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati kimataifa.
Kwa mujibu wa tathmini inayofanywa na Benki ya Dunia kila mwaka, nchi za kipato cha chini ni nchi zenye kipato chini ya dola za Marekani 1,025 kwa kila siku.
Nchi zenye kipato cha juu ni nchi zenye kipato cha dola 12,476 za Marekani. Nyingine zote zinazo angukia katikati ya vipato hivyo viwili, huhesabika kuwa nchi zenye kipato cha kati.
Viwango hivyo hufanyiwa marekebisho kila mwaka. Tanzania hivi sasa inaangukia katika kipato cha dola za Marekani 550.
Bado kuna kazi kubwa kufikia kiwango hicho cha kipato cha kati kama ilivyokusudiwa .
Lengo sio tu kuongeza pato la taifa ili nchi ionekane tajiri, bali ni kupunguza umaskini au kutokomeza kabisa umaskini wa kipato
Ili kufanikisha azma hiyo, ni dhahiri kwamba msisitizo wa uwezeshaji na uwekezaji, lazima sasa uelekezwe zaidi katika kundi hilo kubwa la wakulima wadogo waliopo vijijini.
Bila ya kuwapo kwa viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, sekta ya kilimo peke yake haitasimama.
Uzoefu wa zaidi ya miaka 50 umedhihirisha kwamba kilimo peke yake kimeshindwa kumkomboa mkulima kutoka katika ufukara na umaskini.
Zipo sababu nyingi ikiwamo mkulima kutegema jembe la mkono na mvua.Hata kama mkulima mdogo atawezeshwa kwa kupewa zana bora za kilimo, inawezekana mavuno yake yakashindwa kumkwamua kutoka katika lindi la umaskini, iwapo hakutakuwapo kwa soko la uhakika.
Mbali na kilimo duni cha jembe la mkono kinachotegemea majaliwa ya mvua, pia kukosekana kwa viwanda vya kusindika mazao ya kilimo kumesababisha kuwapo kwa umaskini miongoni mwa wakulima wadogo vijijini, kutokana na mazao mengi kupotea baada ya kuvunwa.
Tathmini zilizofanywa na taasisi za kimataifa hivi karibuni zimebaini kwamba, tatizo la upotevu au uharibifu wa mazao mashambani wakati wa kupanda na kuvuna ni kubwa zaidi katika nchi za bara la Afrika kuliko katika mabara mengine.
Barani Afrika, upotevu wa mazao mashambani katika nchi nyingi ni karibu asilimia 25 ya mavuno yote. Kati ya mavuno yaliyotarajiwa kuvunwa, mara nyingi ni robo tatu ya mavuno yote ambayo hupatikana salama.
Hata hiyo robo tatu ya mavuno, nayo bado iko shakani kutokana na wadudu waharibifu na kuhifadhiwa katika maghala ambayo yapo chini ya kiwango.
Baadhi ya mazao, kama vile matunda, mboga za majani na mazao ya mizizi yanapotea mashambani kwa asilimia 50, ikiwa ni mavuno yote ambayo yalitarajiwa kuvunwa (Voices Newsletter, 2006).
Katika nchi za Afrika Mashariki , hasara inayopatikana kutokana na uharibifu au upotevu wa bidhaa za maziwa hufikia wastani wa dola za Marekani milioni 90 kwa mwaka (FAO, 2004) .
Nchini Tanzania, karibu lita zipatazo milioni 59.5 za maziwa ya ng’ombe huharibika kila mwaka, kiasi ambacho ni sawa na asilimia 16 ya mavuno au uzalishaji wote wa majira ya kiangazi na asilimia 25 ya mavuno yote wakati wa majira ya masika .
Hayo yote yanasababishwa kwa kuwa hakuna viwanda vya kusindika bidhaa za maziwa au kutokuwepo kwa zana bora na za kisasa za kuhifadhi maziwa mashambani.
Nchini Kenya, inakadiriwa karibu lita milioni 95 za maziwa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 22.4 zinapotea au kuharibika kila mwaka.
Nchini Uganda karibu asilimia 27 ya mavuno ya maziwa yenye thamani ya dola za Marekani 23 hupotea au kuharibika kila mwaka .
Changamoto iliyopo mbele yetu, ni njia zipi zitakazo tumika katika kuboresha zana za kilimo cha mkulima mdogo na kupunguza kabisa upotevu na uharibifu wa mazao mashambani?