VIDEO: Rostam Azizi, Mbatia wateta na Magufuli Ikulu

Muktasari:

Leo Jumanne Novemba 13, 2018, mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Rostam Aziz, wenyeviti wa vyama vya siasa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), John Cheyo (UDP) na Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa, John Shibuda wamemtembelea Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti


Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Rostam Aziz leo Jumanne Novemba 13, 2018 amemtembelea na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika kipande cha video cha dakika moja, kinawaonyesha wawili hao wakifurahia wakati wakitoka  ndani baada ya mazungumzo yao.

Rostam aliyewahi kuwa mbunge wa Igunga (CCM) amempongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuboresha mazingira ya kufanyia biashara.

Amesema kama mfanyabiashara anatambua juhudi zinazofanyia hivi sasa kwa sababu zinalenga kutengeneza msingi wa uchumi wa uhakika.

“Kinachofanyika sasa ni kuondosha mazingira yasiyo rafiki ili watu waweze kufanya biashara zao kwa haki,” amesema Rostam

Mbali na Rostam,  wengine ambao leo Jumanne wamemtembelea Rais Magufuli Ikulu kwa nyakati tofauti na kufanya naye mazungumzo ni wenyeviti wa vyama vya siasa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), John Cheyo (UDP) na Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa, John Shibuda.