VIDEO: Serikali, Tucta hakijaeleweka nyongeza ya mshahara

Alichokisema MSIGWA kuhusu MISHAHARA baada ya kukutana na TUCTA

Muktasari:

  • Wakati Serikali ikisema inasubiri majadiliano ya vyama vya wafanyakazi, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limesema kesho Jumatano Julai 27, 2022 litapeleka hoja zao kuhusu kutoridhika na utaratibu uliotumika kwenye nyongeza ya mishahara.


Dodoma. Wakati Serikali ikisema inasubiri majadiliano ya vyama vya wafanyakazi, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limesema kesho Jumatano Julai 27, 2022 litapeleka hoja zao kuhusu kutoridhika na utaratibu uliotumika kwenye nyongeza ya mshahara.

Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa amesema leo Jumanne Julai 26, 2022 kuwa viongozi wa Tucta wameomba muda kwenda kujadiliana kabla ya kuzungumza na Serikali.

“Na baada ya mazungumzo ya awali leo, viongozi Tucta wameomba wapate muda wa kwenda kujadiliana na baadaye watakuja kuzungumza na Serikali,” amesema Msigwa.

Amesema viongozi wa Tucta watakapokamilisha majadiliano yao, watakutana na Serikali ili wasikilize hoja zao na baadaye Serikali itatoa maelezo yake.

 “Sasa baada ya hapo tutawaambia kilichojili kwenye mazungumzo hayo ni nini na uamuzi wa Serikali,”amesema.

Ametaka uwepo wa subra wakati Tucta ikijadiliana na kwamba nia ya Serikali ni kujenga hakuna kitu cha kuficha wala kibaya.

Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya amesema leo waliionyesha Serikali ni kwa kiwango gani watumishi na viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini hawajaridhika na utaratibu uliotumika kuongeza mshahara.

“Kwa hiyo tumewakabidhi viongozi wa Serikali na sisi tupo hapa Dodoma, tunaendelea na mchakato wa majadiliano. Kwa leo tumefikia hatua ya kuwaeleza (Serikali) kile ambacho hatukukitegemea kwa ile nyongeza ya Mheshimiwa Rais ya asilimia 23.3,”amesema.

Amesema Serikali imepokea hoja zao lakini wataweka hoja zao katika maandishi na kesho watazikabidhi leo Serikalini ili zifanyiwe kazi kiofisi.

Nyamhokya amesema wafanyakazi walikuwa na furaha na bashasha wakati Rais Samia alivyotangaza nyongeza ya mishahara lakini kwa bahati mbaya kilichotokea katika salary slip zao kimekuwa tofauti na matarajio yao.

Amesema kwa kawaida ilivyozoeleka ni kuwa asilimia ya nyongeza ya mishahara inayotajwa huanzia chini na baadaye kuendelea kupungua kadri mshahara unavyozidi kuwa mkubwa.

Amesema uongezaji wa mishahara si jambo geni lakini wanashangaa staili iliyotumika mwaka huu ya nyongeza hiyo iliyofanyika baada ya miaka saba.

Alipoulizwa kiwango kilichoongezwa, Nyamhokya amesema kwa kima cha chini cha mshahara ambacho ni Sh300,000 wameongezwa asilimia 23.3 kama ilivyotamkwa na Rais Samia na hivyo kiasi kilichoongezeka ni kama Sh70,000.

Hata hivyo, amesema kwa upande wa kima cha juu wengi wa wafanyakazi wamekutana na nyongeza Sh26,000 ambayo baada ya kukatwa kodi inabakia nyongeza ya Sh12,000 na wengine wamejikuta na nyongeza ya Sh8,000.

“Naamini wenzetu wa Serikali wamelipokea na wanakwenda kulifanyia kazi na kwasababu bado tunaendelea na mjadala huu. Tunaendelea kusubiri tuyapate majibu ambayo tunaweza kuyarudisha kwa wafanyakazi. Tuko Dodoma kwa ajili ya suala hilo,”amesema.