VIDEO: Serikali ya Tanzania yatoa ufafanuzi uvaaji wa barakoa

Serikali ya Tanzania yatoa ufafanuzi uvaaji wa barakoa

Muktasari:

  • Serikali  ya Tanzania imesema mtu anaweza kuvaa barakoa ili kujikinga na magonjwa yanayosambaa kwa njia ya hewa ikiwemo kifua kikuu.

Mwanza.  Serikali  ya Tanzania imesema mtu anaweza kuvaa barakoa ili kujikinga na magonjwa yanayosambaa kwa njia ya hewa ikiwemo kifua kikuu.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Februari 5, 2021 na katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Mabula Mchembe alipotembelea  hospitali  za rufaa za Bugando na  Sekou-Toure na kubainisha kuwa hospitali hizo hazina  wagonjwa wa Covid-19 .

Akizungumza na waandishi wa habari leo Profesa Mchembe amewataka wananchi kuondoa hofu ya uwepo wa wagonjwa katika hospitali hizo.

Serikali ya Tanzania yatoa ufafanuzi uvaaji wa barakoa

Akijibu swali kuhusu uvaaji wa barakoa, Katibu mkuu huyo amesema mtu yeyote anayehisi yuko kwenye eneo hatarishi kwa maambukizi ya magonjwa yanayosambaa kwa njia ya hewa ikiwemo kifua kikuu avae barakoa.

“Uvaaji wa barakoa siyo kwa ajili ya kuzuia virusi vya corona kama wengi wanavyofikiria, bali ni kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya maradhi yanayoambukiza kwa njia ya hewa,” amesema.

Akitoa taarifa kwa katibu mkuu huyo kwa nyakati tofauti, Kaimu mkurugenzi wa Bugando, Dk Fabian Massaga amesema hospitali hiyo haina mgonjwa yeyote wa Covid 19 kama inavyodaiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Amesema hospitali hiyo inapokea wagonjwa wenye changamoto ya kupumua inayotokana na maradhi mengine ikiwemo shinikizo la damu, uzito uliopitiliza na kifua kikuu.

Maelezo kama hayo pia yametolewa na mganga mfawidhi wa hospitali ya Sekou-Toure, Dk Bahati Msaki aliyesema hakuna mgonjwa wa corona hospitalini hapo.

“Tunao wagonjwa watano wenye changamoto ya kupumua inayotokana na maradhi mengine,” amesema Dk Bahati.

Pamoja na kukagua utoaji wa huduma, ziara ya Profesa Mchembe Hospitali za Bugando na Sekou-Toure ililenga kupata ukweli iwapo hospitali hizo zina mgonjwa wa Covid 19.