VIDEO: Simulizi ya mtoto wa miaka tisa anayemhudumia bibi mgonjwa

Simulizi ya mtoto wa miaka tisa anayemhudumia bibi mgonjwa

What you need to know:

  • Shamsa Yusuph (9) ambaye kwa umri wake anapaswa kuwa shule, amejikuta akikosa fursa hiyo baada ya kulazimika kubeba jukumu la kumhudumia bibi yake mgonjwa aliyelala kitandani kwa maradhi kwa miaka mitatu sasa.

Mwanza. Shamsa Yusuph (9) ambaye kwa umri wake anapaswa kuwa shule, amejikuta akikosa fursa hiyo baada ya kulazimika kubeba jukumu la kumhudumia bibi yake mgonjwa aliyelala kitandani kwa maradhi kwa miaka mitatu sasa.

Mtoto huyo anayeoonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuelewa mambo na kujieleza kulinganisha na umri wake, ndiye amekuwa mlezi na mhudumu wa bibi yake, Angelina Francis (64) ambaye kwa mujibu wa maelezo ya madaktari anakabiliwa na ugonjwa wa saratani ya shingo la kizazi ambao umefikia hatua ya juu.

EXCLUSIVE: INASIKITISHA mtoto wa miaka tisa aacha shule 2019 ili kumuhudumia bibi yake

Tangu mwaka 2019, mtoto huyo anayemtaja baba yake mzazi kwa jina la Ramadhani Yusufu anayedai kuwa ni askari wa Jeshi la Wanawanchi Tanzania (JWTZ) katika Visiwa vya Zanzibar, amekuwa ndiye tegemeo la bibi yake katika shughuli zote za nyumbani kuanzia usafi, kuchota maji, kupika, kutafuta kuni hadi kumwogesha.

Akizungumza na Mwananchi jana akiwa pembeni mwa kitanda cha bibi yake aliyelazwa katika hospitali binafsi ya Grambah iliyoko eneo la Kilimahewa, jijini Mwanza, Shamsa alisema: “Mimi ndiye nampeleka bibi chooni kujisaidia, namwogesha, namfulia nguo zake, kufanya usafi wa nyumba na vyoo kulingana na zamu yetu kwenye nyumba tuliyopanga.”

Kufika Mwanza 2019

“Nilifika Mwanza mwaka 2019 nikitokea Zanzibar wakati wa likizo ya mwisho wa mwaka baada ya kufunga shule, nilikuja kwa lengo la kumsalimia bibi; lakini kwa hali niliyomkuta nayo nimelazimika kubaki huku huku nikimhudumia,” alisema Shamsa.

Alisema wakati anafika kwa bibi yake mwishoni mwa Novemba 2019, alikuwa ameshaanza masomo akiwa darasa la kwanza katika shule ya msingi Kivulini huku Zanzibar, lakini hajarejea hadi leo baada ya kujikuta ndiye mtu pekee wa kumhudumia bibi yake.

“Baba naye hajaja kunichukua wala kuwasiliana na mimi au bibi tangu nije huku Mwanza,” alisema mtoto huyo akionyesha sura ya huzuni usoni.

Aliongeza; “ “Nimemkumbuka sana baba yangu, ndugu zangu na marafiki zangu wa Zanzibar. Natamani kuwaona, lakini ndiyo hivyo sina mawasiliano na baba tangu nije huku Mwanza kumsalimia bibi.”

Akijibu swali kuhusu alipo mama yake mzazi, Shamsa alisema; “Mama yangu alishafariki dunia, nakumbuka ilikuwa hata kabla sijaanza shule wala kuja Mwanza kumtembelea bibi.”

Hamu ya shule, tiba kwa bibi

“Natamani kwenda shule kama wenzangu, huwa nikiwaona watoto wengine wanakwenda au kutoka shuleni natamani sana kuwa kama wao, lakini siwezi kumwacha bibi yangu peke yake nyumbani bila mtu wa kumpikia, kumfulia na kumpeleka chooni,” alisema Shamsa.

Aliongeza; “Nikimpata mtu wa kunisaidia kumwangalia na kumhudumia bibi nitaenda shule. Nataka nisome, nipate kazi ili nimsaidie bibi yangu kwa kumununulia chakula, nimjengee nyumba na kumtibu hadi apone.”

Hisia ya kutelekezwa

Akizungumza huku akigugumia kwa maumivu, bibi wa mtoto Shamsa, Angelina Francis (64) alionyesha hisia ya kutelekezwa na watoto wake watano walio hai kati ya watoto 11 aliwaozaa.

“Kwanza namshukuru Mungu kwa kumleta mjukuu wangu Shamsa ambaye badala ya lengo lake la kuja kunisalimia, amejikuta akigeuka kuwa tegemeo langu pekee kwa kunihudumia kila kitu,” alisema Angelina huku akionyesha uso wa huzuni na kukata tamaa.

Aliongeza; “Mwanzo nilikuwa nikiishi vema na kwa furaha na familia yangu ya watoto watano walio hai. Tulikuwa tunaishi mtaa wa Ghana, jijini Mwanza kabla ya kuhamia mtaa wa Isamilo ninakoishi sasa. Maisha yalianza kubadilika nilipougua maradhi ya kutokwa haja ndogo na kubwa bila kujitambua.”

Alisema awali watoto wake walikuwa wakimhudumia vizuri, lakini anadhani baadaye walianza kuchoka na kila mmoja kutawanyika kivyake kwenda kutafuta maisha bila kukumbuka nyuma wala kurejea nyumbani hadi sasa. “Nasikia watoto wangu wawili wanaoitwa Florah na Stella wako Katoro huko Geita; wengine watatu sijui walipo,” alisema Angelina.

Alisema baada ya watoto wake wote kuondoka nyumbani, alianza kuuza baadhi ya mali ikiwemo samani za ndani na mavazi kupata fedha za kujitibu na kujikimu kimaisha.

“Nimeshauza nguo na vyombo vyangu vyote vya ndani; tena baadhi ya mali nimeuza kwa bei ya kutupa ikiwemo kuuza doti ya vitenge kwa Sh5,000 ili nipate fedha za kununua japo dawa ya kutuliza maumivu na chakula change na mjukuu wangu.

“Sina kitu tena, hivi sasa nategemea misaada na fadhila za majirani na watu wanaokuja kunisalimia,” alisema.

Alisema kutokana na maradhi yanayomkabili, wakati mwingine akipata fedha ananunua na kuvaa pampasi kumpunguzia mjukuu wake Shamsa adha ya kulazimika kumbadilisha nguo mara kwa mara. Alisema mwaka 2019 alifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Bugando ambako aligundulika kuwa na maambukizo kwenye njia ya haja ndogo na tayari yalikuwa yameanza kuathiri mfuko wa kizazi.

“Mwaka 2019 nilitakiwa kufanyiwa upasuaji, nilikosa fedha baada ya kulipia zaidi ya Sh800,000 za gharama alizopatiwa,” alisema Angelina.

Kabla ya kukutwa na maradhi yaliyomlaza kitandani kwa miaka mitatu sasa, Angelina alikuwa akijishughulisha na ujasiriamali wa kununua na kuuza mpunga na kufuga kuku wa kienyeji.

“Mungu akinisaidia nikapona haraka nitarejea kwenye ujasiriamali. Naamini nitamudu maisha na kumpeleka shule mjukuu wangu, ili atimize ndoto yake ya kuwa askari wa JWTZ kama alivyo baba yake,” alisema Angelina, huku uso ukionyesha tabasamu la matumaini