VIDEO: Sintofahamu kauli za Paul Makonda

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi, Paul Makonda, ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dodoma jana Novemba 2, 2023.

Dar es Salaam. Maelekezo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) yaliyotolewa na Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Paul Makonda kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yameibua utata baada ya kiongozi huyo kutoa kauli nyingine kwamba “chama hakina shaka na utendaji wa Waziri Mkuu.”

Juzi, wakati akipokewa katika ofisi za makao makuu ya CCM jijini Dodoma, Makonda alitoa maelekezo ya chama kwa Majaliwa kuhakikisha anasimamia, kuratibu, kuondoa na kufuta migogoro ya ardhi inayosababisha wananchi wateseke.

Makonda alisema chama kinampa miezi sita kuhakikisha anashughulikia migogoro hiyo ya ardhi ambayo imekithiri katika maeneno mengi nchini ikiwa na sura tofauti.

Maelezo hayo yaliibua mijadala maeneo mbalimbali, ikiwemo mitandaoni na wachambuzi wa kisiasa waliozungumza na Mwananchi wakikosoa njia iliyotumika kufikisha maelekezo hayo kwa Waziri Mkuu ambaye pia ni mjumbe wa vikao vyote vya juu cha CCM.

Mjadala huo unajikita pia kwenye hoja kwamba kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Idara ya Itikadi na Uenezi inayoongozwa na Makonda imebainisha majukumu ambayo “haihusiki na kutoa maagizo kama anavyofanya.”

Idara hiyo ina majukumu ya kushughulikia masuala ya msingi ya itikadi na sera za CCM, kueneza na kufafanua itikadi na sera za CCM na kupanga na kusimamia mafunzo na maandalizi ya makada na wanachama.

Sintofahamu kauli za Paul Makonda

Kusimamia vyombo vya habari vya chama, mawasiliano na uhamasishaji wa umma kwa jumla. Kuongoza na kusimamia maandalizi ya sera, programu na Ilani za Uchaguzi za CCM na mwisho kusimamia utafiti, maktaba na nyaraka za chama.

Katikati ya mijadala hiyo, jana, Makonda alikwenda bungeni na kuhudhuria kikao cha asubuhi na baadaye alikutana na Majaliwa ofisini kwake ambapo alisema chama hakina shaka na utendaji wake.

“Katika utendaji wa kazi, sisi upande wa chama tuna matumaini makubwa na uwajibikaji na uaminifu wa Waziri Mkuu, Majaliwa, tumemuona katika maeneo mengi akisimamia shughuli za Serikali na nilipotoa agizo la chama kwa Waziri Mkuu nilitaka agizo hilo lifike kwa mtu anayeweza kuleta matokeo chanya kwa chama,” alisema Makonda kama alivyonukuliwa kwenye taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Taarifa hiyo ilimnukuu Makonda akisema lengo la CCM ni kuhakikisha Serikali inatimiza kile ambacho imepewa kukifanya kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi, hivyo wana matumaini makubwa na utendaji kazi wa Majaliwa.

Kauli hiyo ya Makonda imeibua utata, kwani maagizo aliyoyatoa juzi yalionyesha Majaliwa ambaye ni msimamizi wa shughuli za kila siku za Serikali, hajafanikiwa kutatua migogoro ya ardhi, licha ya kamati ya mawaziri wake wanane kuzunguka nchi nzima.

“Nadhani kauli hii ya Makonda kuhusu Waziri Mkuu kwa kiasi fulani inaonyesha anajisafisha na kubadili gia angani. Ni kauli tatanishi kwa sababu toka mwanzo wachambuzi wengi wa kisiasa walibainisha kuwa Makonda anavuka mipaka ya majukumu yake. “Kwa taratibu za CCM, mtendaji mkuu na msemaji mkuu wa chama ni katibu mkuu. Kitendo cha Makonda kutoa maagizo kwa Waziri Mkuu ni sawa na kusema amepora madaraka ya katibu mkuu wa chama. Hii si ishara njema kwa uhai wa chama na anakigawa chama asipokuwa makini,” alisema mwanazuoni mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina.

Alisema anaamini kwa kauli hiyo mpya, huenda imetokana na maelekezo mapya kutoka kwa mamlaka za juu yake ili atengeneze mazingira ya kusafisha hali ya hewa.

“Asipoelekezwa mipaka yake atasababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama, huenda wengi wakawa na hasira dhidi ya mwenyekiti wa chama kitaifa na kwenda kwenye uchaguzi mkuu wakiwa vipande,” alisema mchambuzi huyo wa mambo ya siasa.

Wakizungumzia kauli ya Makonda kuhusu maagizo kwa Waziri Mkuu, Majaliwa, wachambuzi walisema ingawa Makonda alikuwa na nia njema ya kufikisha maagizo hayo, lakini alitakiwa kufuata mfumo rasmi kama ulivyo utaratibu wa CCM.

“Namna alivyowasilisha mwenezi (Makonda) inatia mashaka kwa sababu CCM hutoa maelekezo kwa mfumo wa press realese (taarifa), lakini namna alivyowasilisha haikuwa taarifa bali alikuwa kwenye hadhara.

“Kuna namna fulani suala hili halijakaa vema, alitakiwa aeleza kwenye taarifa kama ilivyo utaratibu wa CCM kwamba katika kikao kilichoketi siku fulani chama kimeaigiza Serikali… Lakini alivyotamka pale hadharani kwa majigambo si sawa,” alisema Ramadhan Manyeko.

Manyeko ambaye ni mchambuzi wa siasa, alisema inawezekana kweli agizo ni la CCM, lakini namna Makonda alivyoliwasilisha hakufuata utaratibu unaotakiwa. Alisema alivyotoa maagizo hayo ni kama vile Majaliwa yupo kikaangoni.

Wakati Manyeko akieleza hayo, mchambuzi mwingine, Kiama Mwaimu alisema Makonda hakuwa sahihi kutoa maagizo yale hadharani.

“Ni kama vile ametoa amri, alitakiwa kusema chama kinaigiza Serikali sio kutaja majina ingetosha. Masuala haya yangefanyika ndani, kisha taarifa inatolewa kwa umma, sio vile alivyofanya jana (juzi),” alisema Mwaimu.

Wakati kukiwa na maoni tofauti, Mwananchi lilimtafuta Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Anamringi Macha kupata ufafanuzi kuhusu kauli ya Makonda, hata hivyo hakutaka kuzungumza kwa madai hakuwepo kwenye mkutano wa mapokezi ya Makonda.

“Unajua statement (taarifa) zinapotolewa mahali, kila mmoja anakuwa na tafsiri yake au yule anayeandika anaandika anavyoona mwenyewe, hivyo siwezi kutoa ufafanuzi kuhusu hili, kwa sababu sijaingia kiundani na sipo katika nafasi nzuri ya kutoa maelezo,” alisema Macha.

Kuhusu kauli ya Makonda kwamba wastaafu kutulia na kama watahitajika wataitwa, mchambuzi mwingine, Kiama Mwaimu alisema, “katika tamaduni zote huwezi kuzungumza hivi kwa waliostaafu, wamestaafu haijalishi wamefanya vizuri au vibaya, unachotakiwa ni kuchukua mawazo yao kama unataka, kama hutaki acha, lakini uache wazungumze ilimradi wasitukane au kuvuka mipaka.”

Hata hivyo, mchambuzi wa masuala siasa, Ali Makame amekuwa na maoni tofauti akisema: “Kawaida unapokuwa mstaafu unatakiwa kumpumzika, mfano ulikuwa waziri mkuu, lakini kila siku unaanza kujisemea kama waziri mkuu au ulikuwa mwenyekiti, lakini kila siku unazungumza kama mwenyekiti wakati kuna mwenyekiti mwingine.

“Mambo haya yanaweza kuleta chokochoko na kuzua sintofahamu, lakini ustaarabu uliopo Tanzania kila anayestaafu akihitajika anaitwa. Sasa kila mstaafu akisema ile dhana ya kustaafu haitakuwepo,” alisema.