VIDEO: Uenyekiti wa Chadema wamng'oa mbunge Ukonga
Muktasari:
- Waitara, aliyekuwa mbunge wa Ukonga, anafuata nyayo za mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel kuihama Chadema na mbunge wa tatu kuhamia CCM baada ya mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia kuihama CUF Desemba mwaka jana.
Dar es Salaam. Mwita Waitara amekuwa mbunge wa pili ndani ya mwaka mmoja kuihama Chadema na kujiunga na CCM, akisema nia yake ya kugombea uenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani iligeuka shubiri.
Waitara, aliyekuwa mbunge wa Ukonga, anafuata nyayo za mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel kuihama Chadema na mbunge wa tatu kuhamia CCM baada ya mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia kuihama CUF Desemba mwaka jana.
Dk Mollel na Mtulia walipewa tena fursa ya kusimama kugombea ubunge wa majimbo yao baada ya kuyaacha kwa maelezo kuwa wanamuunga mkono Rais John Magufuli.
Waitara alitangaza uamuzi wake huo jana katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam, akiwa sambamba na katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole.
Alisema sababu za kujiuzulu ni pamoja na kuhoji suala la matumizi ya ruzuku na hoja yake ya kutaka mwenyekiti wa Chadema awe anabadilika, ambayo anadai ilifanya achukiwe na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe aliiambia Mwananchi kuwa hakuwahi kumtishia Waitara na kwamba hata mchakato wa kugombea uenyekiti wa chama hicho, haujatangazwa na wala hakuna aliyejitokeza.
“Sitegemei mtu akiondoka Chadema akamsifu Mbowe, lazima atarusha mawe kwenye mti wenye matunda,” alisema Mbowe.
‘Huruhusiwi kuhoji’
Akieleza sababu za kujitoa Chadema, Waitara aliyeingia ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo za CCM kwa kushtukiza, alikiri kutaka kuwania uenyekiti.
“Ukiwa Chadema, huruhusiwi kuhoji chochote,” alisema.
“Ugomvi wangu na Mbowe ni kwa sababu kuna uchaguzi wa chama. Mimi nilisema huyu mtu ameongoza kwa miaka 20 ni umri wa mtu mzima na chama kinaitwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo. Sasa nilipohoji hilo jambo nilipata matatizo makubwa,” alisema Waitara.
Waitara aliyejiunga na CCM mwaka 1998 na kuachana nayo mwaka 2008 wakati wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime, alisema uenyekiti ndiyo tatizo.
“Ukianzia kwa akina Chacha Wangwe (mbunge wa zamani wa Tarime, Chadema), (kiongozi wa ACT Wazalendo) Zitto Kabwe, hata mimi ni uenyekiti. Hapo kuna shida.
“Kuna kikao tulikaa na wabunge wengi wa majimbo na viti maalumu tukawa tunazungumza kwamba Tundu Lissu agombee uenyekiti. Baadaye (wengine) wakaicha hoja hiyo, mimi nikaendelea nayo. Wakaniuliza ninataka Tundu Lissu agombee au ni mimi mwenyewe?
“Mbowe amewahi kuniambia kamanda unanipinga na mimi nitakushughulikia na kwenye Chadema bado hakuna mtu kama yupo nitamng’oa. Hiki chama ni mali yangu.” Alitaja sababu ya pili kuwa ni matumizi ya ruzuku ambapo alidai licha ya kupata Sh236 milioni kwa mwezi, Chadema haina ofisi ya makao makuu, haina ofisi ya kanda, haina ofisi ya mkoa, haina ofisi ya jimbo na haina watumishi wake.
“Jimbo la Ukonga lina mahitaji mengi. Tuna shida ya maji, umeme na afya na ujasiriamali kwa vijana. Hizi kazi zinahitaji ushirikiano mkubwa sana ili kuzitatua kero,” alisema.
Hata hivyo, alisema maendeleo hayana chama na kwamba amehamia CCM ili kurahisisha uletaji wa maendeleo jimboni kwake.
Akizungumza na tuhuma hizo, Mbowe alisema wakati Waitara anajiunga Chadema aliitukana CCM na sasa amegeuka. “Sijawahi kumzuia Waitara kuzungumza na viongozi wa CCM. Mimi ni mbunge naelewa kazi zetu ni lazima kujichanganya na viongozi kama mawaziri. Nitamzuiaje. Huo ni ujinga,” alisema.
“Waitara alikuja Chadema tukampokea, hakushinda kwenye kura za maoni alikuwa wa tatu, lakini chama kikambeba halafu leo anaitukana Chadema? Siwezi kuyumbishwa naye, namtakia safari njema.”
Zitto alishangaa Waitara kuihama Chadema wakati viongozi wa chama hicho wakiwa katika misukosuko ya polisi, hospitali wakiuguza majeraha ya kushambuliwa kwa risasi, huku wanachama wakikamatwa na polisi.
Katika akaunti yake kwenye mtandao wa Twitter, Zitto anamshangaa Waitara kuchukua huo wakati “mbunge mwenzio yupo hospitali mwaka sasa kwa majeraha ya risasi kufuatia jaribio la kumuua. Viongozi wa chama chako karibu wote ngazi ya Taifa wana kesi inayohatarisha kuwaweka jela” na kuhoji kama alitafakari hayo.