VIDEO: Viongozi Chadema wamlilia Mwanakotide

Muktasari:

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania wamesema kifo  Fulgence Mapunda maarufu Mwanakotide ni pigo kwa chama hicho kutokana na umuhimu aliokuwa nao

Dar es Salaam. Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania wamesema kifo  Fulgence Mapunda maarufu Mwanakotide ni pigo kwa chama hicho kutokana na umuhimu aliokuwa nao.

Mwanakotide, kada wa Chadema alifariki dunia Jumapili Oktoba 6, 2019 katika Hospitali ya St Monica, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa.

Alikuwa mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za hamasa za chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, kujizolea umaarufu kupitia mikutano ya hadhara ya chama hicho, zikiwemo kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na 2015.

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema Mwanakotide atakumbukwa kwa alama aliyoiweka katika chama hicho kwa zaidi ya miaka 15.

Amesema alikuwa na mchango kwenye chama na ataendelea kuishi miongoni mwa wana Chadema kwani katika nyimbo maarufu ambazo zilileta ‘amsha amsha’,  Mwanakotide ndio alikuwa mtunzi na mwimbaji.

“Ukiusikiliza wimbo wa Chadema Peoples Power na nyinginezo, lakini pia ameshiriki sana kwenye hamasa na kukielezea chama amekuwa akishiriki katika ziara nyingi za kichama ni mtu ambaye ana jina kubwa sana tumepata pigo na tumepoteza mtu muhimu sana,” alisema Mshinji.

Naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar),  Salum Mwalimu amesema “Unaweza ukaona namna gani CCM  kilivyopata umaarufu kupitia kundi lake la TOT na hivyohivyo Mwanakotide amekuwa nguzo muhimu katika sanaa na burudani katika kueneza itikadi, falsafa na ilani ya chama cha Chadema, ameifanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa sana amekuwa mhamasishaji.”