Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vifaatiba vya Sh95 milioni kuimarisha kambi ya matibabu

Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dk Ntuli Kapologwe (kulia), akimkabidhi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Emmanuel Tayari, vifaa tiba, dawa na bidhaa za afya vyenye thamani ya dola za Marekani 36,000 (Sh95 milioni) kwa ajili ya Kambi ya Huduma za Kibingwa na Upasuaji Maalumu, katika hafla iliyofanyika jijini Arusha, Julai 20, 2026. 

Muktasari:

  • Kambi ya huduma za kibingwa na upasuaji maalumu itakayoanza Julai 20 hadi 30, 2026 mkoani Arusha na Mtwara kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wa nchi wanachama ECSA.

Arusha. Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC) imeikabidhi Serikali ya Tanzania vifaatiba, dawa na bidhaa za afya vyenye thamani ya dola 36,000 za Marekani (Sh95 milioni) kwa ajili ya kambi ya huduma za kibingwa na upasuaji maalumu itakayofanyika kuanzia Julai 20 hadi 30, 2026.

Kambi hiyo, iliyoratibiwa kwa ushirikiano kati ya ECSA-HC na Wizara ya Afya, itafanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mount Meru, Arusha na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, Mtwara.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo jijini Arusha leo Jumatatu, Julai 20, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC, Dk Ntuli Kapologwe amesema mpango huo unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotekeleza mpango huo, huku ukitarajiwa kuendelea katika Kenya, Mauritius na nchi nyingine wanachama baada ya Malawi na Uganda.

Dk Kapologwe amesema kambi hiyo itasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji upasuaji maalumu, kupunguza muda wa kusubiri huduma za kibingwa na kuongeza uwezo wa wataalamu wa afya kupitia kubadilishana uzoefu na utaalamu.

Aidha, amesema vifaa vilivyotolewa vitaendelea kutumika katika hospitali husika hata baada ya kambi kumalizika, hivyo kuacha mchango wa kudumu katika kuboresha huduma za afya.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Serikali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Emmanuel Tayari amesema makabidhiano hayo yanaonyesha mafanikio ya ushirikiano wa kikanda katika kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.

“Hatupo hapa kupokea msaada pekee, bali kupokea wajibu wa kuhakikisha vifaa hivi vinatumika kwa uwazi, uwajibikaji na kwa malengo yaliyokusudiwa,” amesema.

Amesema kambi hizo zitatoa huduma za matibabu na wakati huohuo kuwa jukwaa la kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa Tanzania kupitia ushirikiano na wenzao kutoka nchi nyingine za ECSA-HC.

Mwenyekiti wa maandalizi ya kambi hiyo ambaye ni  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Dk Mpoki Ulisubisya amesema madaktari bingwa na wabobezi 33 wamewasili Arusha kwa ajili ya kutoa huduma hizo, huku wengine wakielekea Mtwara.

Amesema zaidi ya wagonjwa 229 wamejiandikisha Arusha na 251 Mtwara, huku kila kambi ikitarajiwa kuhudumia zaidi ya wagonjwa 1,000 na zaidi ya 500 kufanyiwa upasuaji wa magonjwa mbalimbali yakiwamo ya masikio, pua na koo, mifupa, uzazi na saratani.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea, amesema kambi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, kupunguza rufaa zisizo za lazima na kuhakikisha Watanzania wanapata matibabu bora ndani ya nchi kwa gharama nafuu kupitia ushirikiano wa kikanda.