Vifo ajali ya daladala Kagera vyafika sita
Muktasari:
Ajali hiyo ilitokea jana Desemba 5, 2023 na kusababisha vifo vya watu wanne huku wengine 21 wakijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu
Bukoba. Idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya daladala iliyotokea eneo la Kyetema Barabara Kuu ya Biharamlo - Bukoba imefikia sita baada majeruhi wawili waliokimbizwa kwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kufariki dunia.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Desemba 6, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amesema waliofariki dunia wakati wakiendelea kupatiwa matibabu ni kati ya majeruhi 21 waliokimbizwa hospitalini baada ya ajali hiyo.
"Kutokana vifo hivyo viwili, majeruhi waliosalia hospialini wanaoendelea kupatiwa matibabu sasa ni 19," amesema Sima
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda amesema japo uchunguzi wa kina unaendelea kubaini chanzo cha ajali hiyo, taarifa za awali zinaonyesha kuwa kabla ya ajali, gari hilo lilikuwa kwenye mwendo kasi wakati likiteremka kwenye mteremko wa Kyetema.
Ajali hiyo ilitokea jana Desemba 5, 2023 na kusababisha vifo vya watu wanne huku wengine 21 wakijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Eneo la Kyetema una mteremko mkali na mara nyingi baadhi ya madereva wa magari ya abiria huondoa gia na kuachia gari likiserereka lenyewe, hali inayoongeza uwezekano wa kushindwa kudhibiti gari kwa wepesi dharura yoyote inapotokea.