Miili ya askari waliofariki ajalini yaagwa

Muktasari:

  • Miili ya askari polisi wawili waliofariki dunia jana katika ajali ya gari iliyotokea Kijiji cha Isoliwaya wilayani Wanging'ombe imeagwa leo tayari kwa safari ya Mbeya na Tanga walikotokea.

Njombe. Miili ya askari Polisi wawili waliofariki dunia jana katika ajali ya gari iliyotokea Kijiji cha Isoliwaya wilayani Wanging'ombe, mkoani Njombe, imeagwa leo katika viwanja vya idara ya maji wilayani hapa.

Akitoa salamu za rambirambi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amesema askari hao wamekutwa na mauti wakiwa anatekeleza majukumu yao ya kila siku. Amewataja askari hao kuwa ni  Elizabia Kizale (35) mwenyeji wa Mbeya na Patrick Salehe (34) wa mkoani Tanga.

"Askari hawa walipata ajali jana eneo la Isoliwaya wakati wanaelekea kazini kutekeleza majukumu yao, hivyo hatuna budi kuwaombea," amesema Kamnda Banga na kuongeza;

“Miili yao inasafirishwa leo kuelekea nyumbani kwao katika mikoa ya Mbeya na Tanga ambako ndiko walipotokea kwa ajili ya taratibu nyingine za mazishi. Nitoe wito kwa madereva kuwa makini na kuzingatia sheria wanapokuwa wanaendesha vyombo vya moto ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.

Kwa upande wa Padri wa Kanisa Katoliki, Tarcisio Moreschi ambaye ameongoza ibada hiyo, amewata waumini wa kanisa hilo kumrudia Mungu na kufanya mema wakati wote wawapo dunia. “Tunapaswa kumuomba Mungu wakati wote kwani hatujui siku wala saa ya Mungu kutuchukua.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe, Claudia Kitta kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema amepokea taarifa ya msiba wa askari hao kwa masikitiko makubwa, kwani kifo kimewakuta wakiwa wanatekeleza majukumu yao.

"Askari hawa wamekuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa na tabia nzuri hivyo sisi tunaosalia tuendelee kuiga mfano huo katika utendaji wa kazi," amesema Kitta.

Baadhi ya askari walioshiriki katika ibada hiyo akiwemo Franco Malimba, amesema kifo cha wenzao kimewahuzunisha na kwamba hawana la kufanya zaidi ya kuwaombea kwa mungu.