Wanne wafariki dunia, 21 wajeruhiwa Kagera

Gari lilolopata ajali katika eneo la Kyetema barabara kuu ya kutoka Biharamulo kupita Bukoba kwenda Mtukula na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi 21.

Muktasari:

  • Gari dogo aina Toyota Hiace limepata ajali maeneo ya Kyetema na kusababisha vifo vya watu wanne huku wengine 21 wakijeruhiwa.

Bukoba. Watu wanne wamefariki dunia na wengine 21 wakijeruhiwa baada ya gari dogo aina ya Toyota Hiace iliyokuwa ikitokea Katoro Bukoba Vijijini, kuelekea Bukoba Mjini kupata ajali chanzo kikitajwa  ni mwendokasi.

Akithibitisha juu ya ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda amesema ajali hiyo imetokea leo Desemba 05, 2023 saa 11:30 asubuhi katika eneo la Kyetema barabara kuu ya lami itokayo Biharamulo kwenda Bukoba kupita kwenda Mtukula.
"Kati ya marehemu hao, watu wazima ni watatu, huku kukiwa na mtoto mmoja, lakini pia majeruhi 21 ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wanaendelea na matibabu, kati yao; watoto ni wanne huku watu wazima wakiwa 17,” amesema Chatanda.
“Katika majeruhi hao, wapo ambao hali zao siyo nzuri, huku wengine wakiendelea vizuri. Chanzo cha ajali ni mwendokasi. Uchunguzi wa awali umebaini wakati dereva akishuka mteremko wa Kyetema, aliondoa gia na alipokaribia mwisho wa mteremko alijaribu kuirudisha, haikuwa kwenye mfumo na hivyo kugonga nguzo ya umeme na kusababisha ajali.”

Chatanda ametoa lai kwa madereva kuwa wanapokuwa wamebeba abiria wajue wamebeba roho za watu, wana wategemezi, waache kucheza na vyombo vya moto.