Vifo kutokana na mafuriko Mlimba vyafikia 49

Muktasari:

  • Katika wilaya za Rufiji na Kibiti Mkoa wa Pwani ambazo zilikumbwa na mafuriko ahueni imeanza kupatikana baada ya maji kupungua hasa katika Mto Rufiji kutokana na kupungua kwa mvua kwenye mikoa yenye mito inayoingiza maji kwenye mto huo.

Dar es Salaam. Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema idadi ya vifo vilivyotokana na mafuriko katika Halmashauri ya Mlimba, mkoani Morogoro imefikia 49.
 Msemaji wa Serikali ameeleza hayo leo Aprili 20, 2024 jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa juu ya hali ya mafuriko nchini na ratiba ya sherehe ya Muungano itakayofanyika Aprili 26, mwaka huu.
  “Eneo la bonde la Mto Kilombero limepata mafuriko zaidi kuliko Bonde la Mto Rufiji, na kutoka Mto Kilombero ndiko asilimia 62 ya maji ya Mto Rufiji hupatikana,” amesema Matinyi.

Matinyi amesema halmashauri mbili za mkoa huo wa Morogoro za Mlimba na Ifakara zimeathirika zaidi na kuna kambi sita zilizohifadhi waathirika 1,500 wa mafuriko hayo.
 Kuhusu nyumba, msemaji huyo wa Serikali amesema zilizobomoka mpaka sasa zimefikia 1,276 na zilizozingirwa na maji ni 7,731.
 Ameongeza, “ekari za mazao mbalimbali 97,545.9 zimeathirika za mkoani Morogoro.”
 

Pwani yapata ahueni

Matinyi amesema Mkoa wa Pwani katika Wilaya za Rufiji na Kibiti ambazo zimekumbwa na mafuriko ahueni imeanza kupatikana kwa mafuriko kupungua, hasa katika Mto Rufiji kutokana na kupungua kwa mvua kwenye mikoa yenye mito inayoingiza maji kwenye mto huo.
 “Kata 17 za Rufiji na Kibiti ndizo zimeathirika, tuna kambi sita ya makazi ya muda yenye watu 2,883,” amesema.
 Katika eneo hilo kaya 29,510 zenye watu 125,668 ndizo zimepata athari, miundombinu ya afya, shule, mifumo ya maji na barabara pia imeathirika, amefafanua msemaji huyo.

Amesema mashamba yaliyoathirika ni jumla ya ekari 105,296.24 na mengi yakiwa ni ya mazao ya chakula.
 Mkoani Mbeya nayo, msemaji huyo wa Serikali amesema mafuriko yameuathiri pia na nyumba 20 zimeathiriwa na maporomoko ya tope kutoka Mlima Kawetere, Kata ya Itesi.

Amesema maeneo yaliyoathiriwa ni ya Mwasote na Gombe Kaskazini.
 “Madhara hayo yamesababisha kaya 27 zenye watu 96 kukosa makazi, hivyo Serikali ya mkoa imeanzisha kambi kwa ajili ya kuwatunza wananchi hao,” amesema.
 Kwa mujibu wa Matinyi, Serikali imeshapeleka wataalamu wa jiolojia kwenda kuchunguza chanzo cha tukio hilo.
 “Udongo ambao kwa kiasi kikubwa unatokana na majivu ya volkano ya kutoka vitovu vya Rungwe na Ngozi zaidi ya miaka 1,250 iliyopita, ndio unaunda Mlima wa Kawetere, unachanganyikana na udongo wa mfinyanzi ambao haujashikamana vizuri na kwa muda mrefu umekuwa ukipata mvua na kutota na hatimaye kufikia kiwango kilicholeta athari,” alisema Matinyi.
 Mlima huo pia una chemchemi ya maji inayotiririka majira yote, alisema.