Vifo vyafikia 20 mafuriko Hanang

Hali ilivyo kwenye mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang' Mkoani Manyara baada ya kutokea mafuriko.

Muktasari:

  • Vifo vilivyosababishwa na mafuriko katika eneo la Katesh na Gendabi wilayani Hanang mkoani Manyara, vimefika 20 huku majeruhi wakiwa 70, taarifa za awali zinasema kuporomoka kwa sehemu ya Mlima Hanang ndio chanzo cha mafuriko hayo.

Arusha. Mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia leo Jumapili Desemba 3, 2023 mkoani Manyara imesababisha mafuriko ya tope katika eneo la Katesh na Gendabi wilayani Hanang na kuua watu 20 na kujeruhi 70 mpaka mchana wa leo Jumapili, Novemba 3, 2023.

Taarifa kutoka kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanadai kuwa mvua hiyo imesababisha kuporomoka kwa sehemu ya Mlima Hanang na kusababisha vifo hivyo ambavyo kuna uwekezano vikaongezeka.

Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja akizungumza na Mwananchi Digital, Leo, Jumapili Novemba 3, 2023 amesema hadi mchana (saa 7.30) miili 20 imepatikana na majeruhi 70 wanatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tumaini.

"Uokoaji unaendelea katika maeneo ya Katesh na Gendabi ambapo mafuriko hayo yamepita na kusomba nyumba kadhaa, maeneo ya biashara na kituo kikuu cha kabasi cha Katesh, vifo mpaka sasa vimefika 20,"amesema

Amesema uakoaji unaendelea kufukua tope ambalo limefunika nyumba, maduka na maeneo mbalimbali.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hanang, Rose Kamili amesema zoezi la uokoaji bado ni gumu kwani kuna maeneo mengi hayafikiki.

"Mimi nipo eneo la tukio hali sio nzuri kuzunguka mlima Hanang na tunaendelea na zoezi la uokoaji,"amesema

Jeremiah Siay mkazi wa Katesh amesema ndugu zake wawili ana hofu wamesombwa na mafuriko kwani hawajulikani walipo.

"Tunahangaika kuwatafuta ndugu zangu na majirani hali sio nzuri mlima umepasuka na kuanza kushusha Maji chini,"amesema.

Amesema mafuriko hayo kutoka mlima yamevunja majumba,  mifugo imesombwa na kuharibu mali nyingi.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga na ujumbe wake waliokuwa ziarani wilayani Kiteto kikazi wapo njiani kwenda wilayani Hanang.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi.