Vijana wa JKT waonywa kutojiingiza kwenye dawa za kulevya

Baadhi ya vijana wa Kujitolea Operesheni Jenerali Venance Mabeyo katika kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa 822 Rwamkoma Butiama mkoani Mara katika gwaride la kuhitimisha mafunzo ya awali ya kijeshi.

Muktasari:

  • Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele amefunga shughuli ya uhitimishaji wa mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa kujitolea Operesheni Jenerali Venance Mabeyo huku akiwaasa kuishi kiapo cha utii, maadili, uaminifu, upendo na uhodari.

Butiama. Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele amewaonya vijana wa JKT kutojiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwasababu wakibainika watasitishiwa mikataba yao.

 Meja Jenerali Mabele ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 17,2023 wakati akihitimisha mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa kujitolea Operesheni Jenerali Venance Mabeyo katika kikosi cha Rwamkoma JKT mkoani Mara.

Amesema madawa ya kulevya yapo ya aina nyingi sana lakini miongoni mwa dawa za kulevya ni bangi na kuwataka kujiepusha na matumizi ya dawa hizo.

“Tukigundua, ikiwa ni bahati mbaya katika kipindi tulichokaa na wewe (katika mafunzo ya awali ya kijeshi), hatukugundua kwamba unatumia dawa hizo, tukajagundua hufai kuwa kijana wa Jeshi la Kujenga Taifa, tutasitishia mkataba wako na kukurudisha nyumbani,”amesema.

Amesema kwa wale wenye tabia nzuri ikitokea nafasi katika chombo chochote ndani ya Tanzania kinahitaji vijana basi hawatasita kuwapendekeza ili wakafanye kazi huko.

Pia Meja Jenerali Mabele, amewataka vijana hao kuendelea kuyaishi yale maisha waliofundishwa wakiwa katika mafunzo hayo na siku zote wawe na umoja kwa kuhakikisha wanapendana wenyewe, ndugu, majirani, Taifa na bara la Afrika.

Naye Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU), Kanali Makame Daima, amewapongeza vijana hao kwa kuhitimu mafunzo yao na kuwataka kwenda kukiishi kiapo chao.

Awali akitoa taarifa ya mafunzo hayo ya awali ya kijeshi, Mkuu wa Tawi la Mafunzo JKT, Kanali Aisha Matanza amesema vijana hao wanawakilisha vijana wenzao katika makambi yote yaliyoendesha mafunzo hayo.

"Haya mafunzo pamoja na kulenga kuboresha nidhamu ya vijana lakini pia watakuwa na uelewa mpana juu ya masuala mazima ya uwajibikaji na uadilifu kwa Taifa," amesema Kanali Matanza.

Akitoa taarifa ya mafunzo Kamanda wa Kikosi cha Rwamkoma JKT, Luteni Kanali Gaudensia Mapunda amesema vijana wa kujitolea Operesheni Jenerali Venance Mabeyo yalifunguliwa Novemba 28,2022 na yalichukua majuma 16.