Vijana waaswa wasijiunge makundi ya uhalifu

Waumini wa dini ya Kiisilamu wakishiriki kwenye ibada ya Siku ya Eid-El-Fitri iliyofanyika kwenye msikiti wa Gadafi jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Shekh wa Mkoa wa Iringa Said Abri amewataka vijana kutafuta kazi halali badala ya kujiunga na makundi ya uhalifu yakiwamo ya ‘Panya Road’.
  • Katika maadhimisho hayo ya Sikukuku ya Eid –El-Fitri, Shehe wa Mkoa wa Katavi, Mashaka Kakulukulu amewahimiza waumini wa dini ya Kiislaam mkoani humo kuitumia kupinga vitendo vya ukatili.

Mikoani. Shekh wa Mkoa wa Iringa Said Abri amewataka vijana kutafuta kazi halali badala ya kujiunga na makundi ya uhalifu yakiwamo ya ‘Panya Road’.

Akizungumza katika wakati wa ibada ya sikukuu ya Eid El Fritri ambayo kwa mkoa wa Iringa imefanyika kwenye uwanja wa Samora, Shekh Abri amesem matukio yote ya kihalifu hufanywa na watu wasio na hofu ya Mungu.

Shekh wa Mkoa wa Iringa, Said Abri

“Iringa tuwe mfano, naomba vijana msijiingize kwenye makundi ya kihalifu, fanyeni kazi,” amesema Shekh Abri.

Awali, akitoa mawaidha, Mjumbe wa Baraza la Mashekh la Mkoa wa Iringa, Yasin Mdesa aliwataka waumini wa dini hiyo kuendeleza matendo mema hata baada ya kumaliza mfungo.

“Mafunzo tuliyopata ndani ya mwezi Mtukufu wa Ramashan tunapaswa kuishi nayo wakati wote, kuweni na subira kwenye kila kitu. Kuwa na subira ni kutekeleza ibada na kila kitu kwenye maisha,” amesema.


Kupinga vitendo vya ukatili

Katika maadhimisho hayo ya Sikukuku ya Eid –El-Fitri, Shehe wa Mkoa wa Katavi, Mashaka Kakulukulu amewahimiza waumini wa dini ya Kiislaam mkoani humo kuitumia kupinga vitendo vya ukatili.

Kakulukulu ametoa rai hiyo kwenye swala ya Eid iliyofanyika viwanja vya Kashato mjini Mpanda.

Amewasihi Waislaamu kuwa na tabia njema zilizotukuka, kuishi na watu vizuri, kupinga mauaji yanayofanywa na watu walioingiwa na roho ngumu.

“Leo tunashuhudia mauaji ya kikatili ya aina mbalimbali yanayotokea sehemu tofauti, hili linatokana na sababu ya kuacha suala la tabia njema,”amesema Kakulukulu.

Amesema suala la tabia njema halioti kama uyoga isipokuwa linaanza mtu akiwa na umri mdogo hivyo wazazi na walezi wanatakiwa kuanza kuwalea na kuwafundisha watoto maadili mema.

“Tukitekeleza hili vizuri itaepusha majanga tunayoshuhudia ya mauaji ya kikatili na chanzo chake ni kukosa hofu ya Mwenyezi Mungu, turejeshe hofu yake na kila mmoja awe balozi kumuasa mwingine,”amesema.


Watakiwa kuendeleza mema

Shekhe Said Ally Hassani kutoka Malindi Nchini Kenya kwa niaba ya Imamu wa Msikiti Sunn Shekh Ahmed Zuberi amewataka waisalamu jijini Dodoma kuendeleza matendo mema kama waliyokuwa wakitenda kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Amesema waislamu katika kipindi cha siku 30 za mfungo wamekuwa na hofu ya Mungu na kutekeleza ibada kikamilifu na kiutenda mambo yenye kumpendeza Mungu.

Pia, Shekhe Said ametoa rai kwa waislamu kuliombea Taifa la Tanzania kuendelea kuwa na Amani.

 “Tumemaliza Ramdhani kwa kuhitimisha siku 30, nawaasa tuendelee kumcha Mungu, sio kwa mwezi wa Ramdhan tu bali katika maisha yetu ya siku zote, namuombea kwa Mungu  Rais wetu wa Tanzani Samia Sulluhu Hassani awe na afya njema ili aendelee na kuwapambania wananchi katika kuhakikisha usalama wa maisha yao” amesema Shekh Saidi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa msikiti wa Masijidi Sunni mjini Dodoma, Shekh Abdul Musa Ally Kombo amewaomba waislamu wajiandae na Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 3, 2022.


Kufuata mafundisho ya dini

Imamu wa msikiti mkuu wilayani Handeni Mkoa wa Tanga, Alhaj Sheikh Ali Mjaila amewameshauri Watanzania kajifunze na kufuata mafunzo ya dini ili kuepuka matendo mabaya yakiwamo mauaji.

Amesema matukio ya mauaji yanatokana na watu kukosa imani na kutokufuata mafundisho ya dini.

Sheikh Mjaila amesema endapo kila kiongozi wa dini, familia na jamii kwa pamoja wakisisitiza watu kujifunza dini itasaidia kupunguza matukio ya mauaji ya mara kwa mara yanayotokea.

"Tunamaliza mwezi wa Ramadhani huu sio mwisho wa kufanya mambo mema, tunatakiwa kufanya mema lakini pia tujifunze dini zetu ili kuepusha matukio kama haya ya watu kuuwana na wengine kujiua, kwa miongozo ya dini zote kuuwa na kujiua ni dhambi", amesema Sheikh Mjaila.

Wakati huo huo Imamu msikiti wa Irishad wilayani Handeni mkoani Tanga Shiekh Muharam Ally amewataka watanzania kuendelea kuilinda amani iliyopo.

"Tukumbuke kuwasaidie wenye mahitaji kwani bado wataendelea kuhitaji msaada wetu, pia tumuombe mungu aendelee kumlinda rais wetu na nchi kwa ujumla kwani bila amani hakuna lolote linaweza kufanyika", amesema Sheihk Muharam.

Imendikwa na Tumaini Msowoya (Iringa), Mary Clemence (Katavi), Shakila Nyerere (Dodoma) na Rajabu Athumani (Tanga)