Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jumla ya Sh987.7 milioni kumaliza kero ya maji vijiji vya Ng’ang’ange, Mdeke

Wananchi wa Kijiji cha Ng'ang'ange wilayani Kilolo wakipunga mikono kupokea mradi wa maji.

Muktasari:

  • Kilio cha kero ya maji kilichokuwa kimewagubika wananchi wa vijiji vya Ng’ang’ange na Mdeke wilayani Kilolo kitamalizika baada ya Serikali kutia saini ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa maji

Iringa. Wakazi wa vijiji vya Ng’ang’ange na Mdeke, wilayani Kilolo Mkoa wa Iringa wanatarajiwa kupata huduma ya maji waliyoikosa kwa miaka mingi baada ya Serikali kutoa Sh987.7 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

Tayari  Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Mkoa wa Iringa na Mkandarasi  Africantric  Co. Ltd  wameshatia saini ya mkataba kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi huo.

Akizungumza leo Jumamosi Mei 18 2024 baada ya utiaji wa saini hiyo, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha  wananchi wake wanapata majisafi na salama.

Amesema hatarajii kuona mradi huo unasuasua na haukamiliki ndani ya muda wa mwaka mmoja uliopangwa ili wananchi waanze kupata huduma hiyo.

“Mradi huu ni miongoni mwa miradi mingi ya maji inayotekelezwa kwenye wilaya hii ya Kilolo, Serikali imeshatoa fedha na kazi inatakiwa ianze mara moja, kilio cha maji sasa kitaisha na maendeleo yataongezeka,” amesema Mathew.

“Serikali haitaki kuwa kikwazo cha wananchi kukosa huduma bora ya maji. Mbali na mradi huu, Serikali imeridhia kuleta visima vya maji vitano hapa Wilayani Kilolo ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji ni uhai.”

Awali, Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga alisema mwaka 2020 wakati anaomba dhamana ya kuongoza jimbo hilo wananchi wa vijiji hivyo waliomba kupatiwa maji, huduma ambayo hawajawahi kupata tangu Tanzania ipate uhuru.

“Uhaba huu wa maji hapa Ng’ang’ange ulikuwa unaniumiza kichwa, nashukuru leo maombi yangu na wananchi hawa yamejibiwa. Mradi huu ni mwarobaini wa kukua uchumi wa vijiji hivi ambavyo wananchi wake hasa wanawake walikuwa wanatumia muda mwingi kutafuta maji,” amesema Nyamoga.

Baadhi ya wanawake wa Ng’ang’ange kulikofanyika mkutano wa utiaji saini wa mradi huo, wamesema bado hawaamini kama maji kwenye vijiji vyao yatatoka.


“Tumehangaika kwa muda mrefu tukichota maji mabondeni, mtu unatembea mpaka kilometa tatu kufuata maji. Unarudi nyumbani ukiwa na ndoo kichwani, dumu mkononi kwa sababu ya uhaba wa maji. Tunashukuru kwa mradi huu japo bado hatuamini kama tutaanza kupata maji ya bomba,” amesema Maria Kalinga, mkazi wa kijiji hicho.

Mkazi mwingine wa Ng’ang’ange Anna John amesema wamekuwa wakichelewa kufanya kazi nyingine za maendeleo kutokana na muda mwingi kuutumia katika kutafuta maji.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilolo, John Kiteve amesema ni matumaini yake mradi huo utakamilika ndani ya muda uliopangwa ili wananchi waanze kunufaika na huduma hiyo.