Vijana wakataliwa kuoa vijiji jirani kisa shida ya maji

Muktasari:

  •  Baadhi ya vijana katika Kijiji cha Muungano wilayani Chemba mkoani Dodoma, wamedai kuwa wanakabiliwa na changamoto ya kukataliwa kuoa katika vijiji vya jirani kutokana na shida ya maji inayowakabili kwa miaka 24.


Chemba. Baadhi ya vijana katika Kijiji cha Muungano wilayani Chemba mkoani Dodoma, wamedai kuwa wanakabiliwa na changamoto ya kukataliwa kuoa katika vijiji vya jirani kutokana na shida ya maji inayowakabili kwa miaka 24.

Kwa mujibu wa wakazi wa kijiji hicho, wanaume wanaotaka kuoa katika vijiji vya jirani wamekuwa wakikataliwa ama kupewa adhabu ya kulima, kukata kuni na kupewa mifugo ya kuchunga ili waweze kuaminiwa kama wanaweza kuishi na wanawake hao.

Akizungumza na Mwananchi Manshwaibu Ramadhani (30) alisema yeye ni miongoni mwa waliokataliwa kuoaa kwa vile wazazi hawataki mtoto wao aende kuteseka kwa kusaka maji hivyo.

“Unakuta mwanamke anakuelewa na mnapendana lakini wazazi wake wanakataa wanasema mtoto wao atakwenda kuteseka kwa kutafuta maji kwa muda mrefu. Suala hili limekuwa tabu kubwa sana kwetu vijana,”alisema.

Naye Mwenyekiti wa kijiji Muhamedi Murisali alisema changamoto hiyo imesababisha wanawake wengi kukimbilia na kuwaacha wanaume wakihangaika na kulea famia.

Alisema wamekuwa wakipishana na wanyama wakali wakiwemo fisi wakati wanaenda kutafuta maji katika mabwawa.

Katibu wa baraza la Waisilamu (Bakwata) Kata ya Kidoka, Bashiru Maulidi alisema wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa vijana kuhusu kukataliwa kuoa katika vijiji vijiji vya Ombiri, Pangalua na Muungano.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara Mbunge wa Chemba (CCM) Mohamedi Monni alisema changamoto hiyo itamalizika baada ya mradi wa maji kukamilika Juni mwaka huu.

Alisema mradi huo ambao umefikia hatua nzuri unajengwa na kwamba Serikali imetoa Sh134 milioni kwa ajili kukamilisha miradi miwili ya kijiji cha Muungano na Chukuruma itakayonufaisha kaya 270.

Imeandikwa na Shakila Nyerere