Vijana waliojitosa BBT kuondoka na mtaji Sh10 milioni
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya mifugo, Profesa Daniel Mushi akizungumza na vijana wanufaika wa mpango wa ‘Jenga Kesho iliyo Njema' (BBT Life) katika Shamba la Mifugo Mabuki lililopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.
Muktasari:
- Katika mafunzo hayo ya mwaka mmoja ya ujasiriamali wa mifugo, kila kijana atatakiwa kunenepesha ng’ombe 10 wakati wa mafunzo na watakapouzwa faida itatumika kama mtaji kwa wanufaika kwenda kuanzisha mradi yao.
Mwanza. Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema kila kijana aliyepo kwenye mpango wa ‘Jenga kesho iliyo njema’ (BBT Life) kwa ajili ya mafunzo ya vitendo katika unenepeshaji wa mifugo na viumbe kwenye maji ataondoka na Sh10 milioni kama mtaji baada ya kuhitimu mafunzo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshugulikia sekta ya mifugo, Profesa Daniel Mushi amesema hay oleo Ijumaa Januari 5, 2024 wakati wa ziara ya kusikiliza kero na mawazo ya vijana hao iliyoanza jana na kumalizika leo katika shamba la mifugo Mabuki lenye vituo atamizi vitatu kati ya vinane nchini.
Kauli hiyo imekuja baada ya vijana zaidi ya 50 waliopo kwenye vituo hivyo kuuliza hatma yao baada ya kumaliza mafunzo Juni, 2024.
“Sisi vijana pamoja na kusoma mwongozo na kujua jukumu la kupata maeneo ya kufanya biashara ya unenepeshaji ng’ombe kama mashamba ya Narco (Ranchi za Taifa) na halmashauri zetu, lakini bado hatujathibitishiwa ni wapi tutakwenda kupata vitalu,” amehoji mnufaika wa BBT, Adelina Bilembo.
Akijibu hoja hiyo, Profesa Mushi amesema licha ya kila mnufaika kuondoka na Sh10 milioni zitakazokuwa mitaji wao wa biashara, pia amesema Serikali itawadhamini kwenye benki kupitia mfuko wa dhamana ya mikopo na kupewa ardhi watakayoitumia kwa miaka mitano.
“Kuna hekta 7,800 zimetengwa na Narco katika ofisi zake mbalimbali ambazo tunatamani nyie mgawiwe kwa utaratibu unaoeleweka, ili muanze kufanya biashara ya unenepeshaji si mna milioni zetu 10 kila mmoja?
“Sasa ile faida ndio itakuwa mtaji wa kuanzia. Ninachotaka kuwaambia vijana wangu ni namna ambavyo mtajipanga kwenye vikundi, si unajua umoja ni nguvu kuliko kwenda kuanza mmoja mmoja? Jipangeni kwenye vikundi ambavyo vina maelewano,” amesema Profesa Mushi.
Ameagiza wasimamizi na waratibu wa vituo hivyo kuwapangia maeneo na ikiwezekana wakaoneshwe kabla ya Machi, 2024 ili watakapomaliza mafunzo wajue mahali wanapokwenda.
Naye Meneja wa Shamba la Mifugo Mabuki, Lini Mwalla amesema vijana hao wakiwa katika vituo hivyo ambavyo ni vya Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (Lita), Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (Taliri) na Mabuki, wanapata mafunzo ya kulisha mifugo, kuandika maandiko ya kibiashara, kuunda vikundi vya ushirika na namna ya kufanya biashara ya mifugo.
Awali, mnufaika wa mradi huo, Bilembo amesema walinunua ng’ombe 900 na kufanikiwa kuuza 557 ambapo wamepata faida ya Sh66,500 kwa kila ng’ombe mmoja, huku gharama ya manunuzi na matunzo ikiwa ni Sh521,000 kwa ng’ombe mmoja.