Vijana wapewa mafunzo ya ujasiriamali
Muktasari:
- Vijana waishio katika mazingira magumu wilayani hapa, wamepewa mafunzo maalumu ya uanzishaji miradi ya kiuchumi itakayowawezesha kuendesha maisha yao na kusaidia familia zao.
Mufindi. Vijana waishio katika mazingira magumu wilayani hapa, wamepewa mafunzo maalumu ya uanzishaji miradi ya kiuchumi itakayowawezesha kuendesha maisha yao na kusaidia familia zao.
Mafunzo hayo yanayojumuisha kata tatu za Igoda , Luhunga na Mdabulo kutoka wilaya ya Mufindi mkoani Iringa yanatolewa kwa kushirikisha vijana hao ambao baadhi yao ni waliokatisha masomo kwa changamoto za maisha wakiwamo mabinti waliopata ujauzito.
Akizungumza Mkufunzi wa mafunzo hayo, John Kalolo kutoka shirika lisilo la kiserikali la RLABS –Tanzania, amesema kuwa mafunzo hayo ni maalum kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa katika ujasiliamali.
"Maeneo mengi ya vijijini kuna fursa nyingi za kufanya ambazo kimsingi ni moja kati ya mtaji mkubwa kwa mtu ambae anatamani kuwa mjasiliamali hivyo iwapo wahusika wataondokana na fikra mgando za kutegemea fedha wanaweza kupiga hatua katika maisha," amesema Kalolo.
Amesema ili vijana hao waondokane na dhana potofu, ni lazima wajitambue kabla ya kuanza shughuli ya ujasilimali na baada ya hapo wanaweza kuomba mikopo ya kuboresha ujasiliamali.
Kalolo amesema ujasiliamali wa ususi kwa wasichana ni kazi ambayo anaweza kuanza kwa ubunifu usio tegemea fedha na ndipo wanaweza kuboresha kwa kutafuta eneo litakalohitaji fedha za kuboresha zaidi.
Kwa upande wake meneja wa mradi wa Youth Agency Mufindi (YAM), Zilipa Mgeni amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha vijana zaidi ya 770 wakiwemo watoto 150 yatima kupata mbinu za kujiajiri.
Amesema mradi huo wa YAM ni wa miaka minne toka mwaka 2021/2024 umefadhiliwa na Serikali ya Finland chini ya taasisi yake ya Diaconess kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania chini ya Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na taasisi ya Foxes Community and Wild Life Conservation.