Vijana wapewa ‘mchongo’ sekta ya kilimo

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu (wa kwanza kushoto) akiongozo mjadala wa kutoa  maoni nini kifanyike kuendeleza Sekta ya kilimo, katika hafla ya 'Uwekezaji Day' ya Benki ya CRDB akifuatiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Equity for Tanzania (EFTA), Nicomed Bohay, Mjumbe wa bodi ya Benki kuu ya Tanzania(BOT) Professa Ester Ishengoma (wa tatu kushoto), Mkuu wa kitengo cha Kilimo na Biashara wa Benki ya (CRDB),Maregesi  Shabani na Mkurugenzi wa Agricom, lex Duffar. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Waaswa kujiunga katika vikundi kujipatia mtaji, uzoefu na elimu kirahisi.

Dar es Salaam. Vijana wametakiwa kujitokeza kuwekeza kwenye sekta ya kilimo kwa kujiunga katika vikundi, ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa urahisi, uzoefu na elimu ya kifedha.

Kwa kufanya hivyo imeelezwa kutasaidia wanafunzi waliosoma masuala ya kilimo kutokimbia fani hiyo.

Mbali ya hayo, imeshauriwa kuboreshwa miundombinu na usafirishaji, kuongezwa mitaji ya uwekezaji, wakopaji kuwa na msukumo wa kulipa mikopo na utengenezaji wa viwanda vya malighafi.

Hayo yameelezwa leo Aprili 28, 2024 katika mjadala ulioendeshwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu uliohusu 'Uwekezaji katika kilimo kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi na ujumuishi wa huduma za kifedha'.

Mkuu wa Kitengo cha Kilimo na Biashara wa Benki ya CRDB, Maregesi Shabani, akizungumza wakati wa hafla ya Siku ya Uwekezaji iliyoandaliwa na Benki ya CRDB, amesema wameshajikita katika kilimo na hakuna atakayeachwa nyuma.

Siku ya Uwekezaji huandaliwa na Benki ya CRDB na hufanyika kila mwaka.

Amesema wamewekeza kwenye Kijani Bond ambayo hadi sasa wametoa Sh500 bilioni.

"Tunatakiwa kubadilisha namna ya uzalishaji kwa hiyo wadau nawaomba muweke msisitizo na mtaji zaidi kwenye elimu ya kilimo, anayewekeza ajue umuhimu wa kuwekeza kwenye teknolojia halisi na mwezeshaji ajue namna ya kutoa fedha kwa yule aliyewekeza," amesema Maregesi.

Amewaomba wawekezaji wote waliopo nchini kuongeza nguvu katika uwekezaji endelevu ambao ni himilivu katika sekta ya kilimo kutokana na mabadiliko ya tabianchi kwani wengi wao wanawekeza kuanzia juu na kuwasahau wale wa chini.

Mjumbe wa Bodi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Esther Ishengoma amesema uwekezaji katika kilimo uondolewe vikwazo, kwani sekta hiyo inahusisha nyingine nyingi hivyo wanatakiwa kuweka mambo mtambuka.

"Uwekezaji wa kilimo umekuwa mgumu kutokana na sheria ya nchi bado haijaruhusu taasisi za pensheni kuwekeza kwenye kilimo, kupunguza changamoto kwenye miundombinu na usafirishaji wa mazao pia wangeshusha gharama za hatifungani ili kuwezesha upatikanaji wa fursa," amesmea Profesa Ishengoma.

Amesema kuondolewe kwa vikwazo katika ardhi ili kuwapa ruhusa wawekezaji kwenye kilimo kupunguziwa changamoto, ikiwemo rushwa na migogoro ya ardhi ambayo huchukua muda mrefu kwenye maamuzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Equity for Tanzania (EFTA), Nicomed Bohay amewataka wanawake kujitokeza kwenye ufugaji na kilimo kwani kumekuwa na unafuu wa mikopo.

"Wapo watu wasiokopesheka kwa sababu hawana mashamba, hususani vijana ambao hawamiliki ardhi lakini sisi tumeingia huko kwa kuwa na matrekta ambayo tumeyapata kwa mkopo na tunawapatia wakulima lengo likiwa ni kuwafikia wakulima wote," amesema.

Akihitimisha mjadala huo, Machumu amesema atahakikisha MCL inatoa elimu kuhusu kilimo na masuala ya fedha kwa jamii.

"Tuliambiwa kuna tabianchi na tabiawatu ili kushughulikia tabiawatu, elimu inahitajika. Kwa pamoja tushirikiane, na sisi Mwananchi Communications hiyo sehemu ya kuelimisha ndiyo yetu mahususi ya kuelimisha watu," amesema Machumu.