Mikopo asilimia 10 kuwatega wakurugenzi wa halmashauri

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipanda mkarafuu baada ya kuweta jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la kitega uchumi cha  Jiji la Tanga lililopewa jina la Dk Samia Suluhu Hassan Business Cetre, eneo la Kange , Aprili 22, 2024.  Wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Buriani. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Muktasari:

  • Majaliwa amesema hayo leo Jumatatu Aprili 22, 2024 jijini Tanga alipokuwa akizungumza na viongozi na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa kitega uchumi kilichopo eneo la Kange, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

Tanga. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameonya halmashauri zote nchini zisizotenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, kuwa zitaanza kuchukuliwa hatua kali.

Amesema wakurugenzi wanapaswa kuwajibika katika hilo kwa sababu ni jukumu lao kutenga fedha hizo.

Majaliwa amesema hayo leo Jumatatu Aprili 22, 2024 jijini Tanga alipokuwa akizungumza na viongozi na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa kitega uchumi kilichopo eneo la Kange, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambacho kilele chake ni Aprili 26, mwaka huu.

Aprili 13, mwaka jana, Serikali ilitangaza kusimamisha utoaji wa mikopo hiyo ya asilimia 10 kwa halmashauri zote nchini baada ya kubaini dosari mbalimbali.

Aprili 16, mwaka huu akiwa bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, alitangaza kuirejesha mikopo hiyo itakayoanza kutolewa kwa mikoa 10 kwa majaribio.

"Kama kuna halmashauri ambayo itakuwa haikuhifadhi fedha hizo, wakurugenzi wake watatafuta kwa kuzipata tunachotaka ni haya makundi yapatiwe mikopo hiyo,” amesema Majaliwa.

Amesema baada ya kufanyiwa maboresho, dosari zilizosababisha kusitishwa kwa mikopo hiyo sasa itaanza kutolewa kwa sababu Serikali inataka kuhakikisha vijana, wanawake na makundi ya watu wenye ulemavu wanajiendeleza kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali ikiwamo uvuvi, ufungaji, kilimo, ufundi na biashara.

Akizungumzia fursa zilizopo mkoani Tanga, Majaliwa amesema Serikali imeweka mazingira bora ya uwekezaji kwa kuimarisha miundombinu ya barabara, reli, bandari na Bahari ya Hindi.

"Wafanyabiashara changamkieni fursa zilizopo Tanga, Serikali imeweka mazingira ya kuufungua mkoa kiuchumi ni mkoa wa kimkakati,ni mkoa muhimu kwa uchumi wa Tanzania,” amesema.

Amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuunda mfuko utakaokuwa na jukumu la kuwawezesha wafanyabiashara, wavuvi, wakulima na wafugaji ili wawe na chombo maalumu kitakachosimamia mikopo yao.

"Tupo katika hatua za mwisho za kuunda mfuko utakaokuwa na jukumu la kuwawezesha kifedha wafanyabiashara, wakulima na wafugaji, tunakamilisha mchakato huo kabla ya kuuwasilisha kwa  Rais Samia Suluhu Hassan, huu utakuwa mkombozi kwa Watanzania,” amesema Majaliwa.

Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Fred Sagamiko, amesema kitega uchumi hicho kimejengwa jirani na stendi kuu, kituo cha daladala, bodaboda na kituo cha maegesho ya malori. 

Amesema mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimi Sh8.7 bilioni mpaka sasa wameshatumia Sh7.4 bilioni kumlipa mkandarasi na Sh544.7 milioni na kiasi kilicholipwa ni Sh7.9 bilioni sawa na asilimia 90.7 ya gharama za mradi.


Mhandisi wa Jiji, Issa Mchezo,  amesema ndani ya kitega uchumi hicho, kutakuwa na ofisi 42 za wakata tiketi za mabasi, eneo la wasafiri kupumzika, maduka, migahawa, vyoo na ukumbi mkubwa wa kufanyia shughuli mbalimbali.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Buriani  amesema mkoa  umepokea Sh2.6 trilioni  kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema Sh259 bilioni zinakwenda kwenye sekta ya elimu ambako shule 27 zimeshajengwa.

“Huku kwenye sekta ya afya tumejenga hospitali sita za wilaya kutoka tatu zilizokuwepo awali,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Amesema Serikali pia imetoa Sh429 bilioni kwa ajili ya kuchimba kina na kuboresha sehemu ya kupakulia shehena ya mafuta katika Bandari ya Tanga.

Upande wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani Tanzania,  umeshaanza sambamba na ujenzi wa bandari maalumu ya kupokea na kupakia mafuta melini.

Katibu wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (Shiuma) Mkoa wa Tanga, Fatuma Mwinyimwaka, amesema mfuko wa kuwawezesha kifedha wafanyabiashara utakuwa mkombozi kwa wajasiliamali, kwani wanakabiliwa na changamoto ya kukosa mitaji.