Vijana wasisitizwa kuongeza ujuzi
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Dk Kedmon Mapana, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kambi ya Mafanikio ya Kitaaluma na Kitaalamu 2026 iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Manispaa ya Morogoro, leo Juni 6, 2026. Picha na Juma Mtanda.
Muktasari:
- Wakati zaidi ya vijana milioni 20 wakiunda zaidi ya theluthi moja ya Watanzania, wataalamu wa maendeleo ya vijana wameonya kuwa shahada pekee haitoshi tena katika soko la ajira linalobadilika kwa kasi kutokana na teknolojia, huku wakitaka uwekezaji mkubwa katika ujuzi wa vitendo na uchumi wa kidijitali.
Morogoro. Zaidi ya vijana 5,000 kutoka vyuo vikuu mbalimbali mkoani Morogoro wamefikiwa na programu za kuwaandaa kukabiliana na changamoto za ajira na kujiajiri, huku ikielezwa kuwa shahada pekee haitoshi tena kumwezesha kijana kufanikiwa katika soko la ajira la sasa.
Akizungumza katika Kambi ya Mafanikio ya Kitaaluma na Kitaalamu 2026 iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) leo Juni 6, 2026 mjini hapa, Mkurugenzi wa Edenconsult Training Center and Accommodation (ETCA), Vicent Gideon, amesema dunia imebadilika kwa kasi kubwa kutokana na maendeleo ya teknolojia, akili unde (AI) na uchumi wa kidijitali, hali inayolazimu vijana kujenga ujuzi unaoendana na mahitaji mapya ya soko.
Gideon amesema takwimu zinaonyesha kuwa vijana ndio nguvu kubwa ya taifa, lakini wengi wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira kutokana na pengo kati ya elimu wanayopata na mahitaji halisi ya waajiri.
“Leo dunia haiulizi una shahada gani pekee, bali una uwezo gani wa kutatua matatizo, kutumia teknolojia na kuleta thamani katika jamii,” amesema Gideon.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Dk Kedmon Mapana, akicheza muziki pamoja na vijana mara baada ya kufungua Kambi ya Mafanikio ya Kitaaluma na Kitaalamu 2026 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Manispaa ya Morogoro, leo Juni 6, 2026. Picha na Juma Mtanda.
Mmoja wa washiriki, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Angela Makoy, amesema mafunzo hayo yamewasaidia vijana kuelewa namna ya kufikia malengo yao ya maisha, ajira na kujiajiri bila kutegemea taaluma walizosomea pekee.
Amesema mafunzo hayo yamegusa masuala mbalimbali muhimu ikiwemo uongozi, ushirikiano, heshima binafsi, kujitambua na namna ya kutumia fursa zilizopo katika mazingira yao.
“Nimevutiwa zaidi na mada iliyowahimiza vijana kuwa jasiri. Hapo awali nilikuwa naogopa kuanzisha biashara, lakini sasa nimejifunza umuhimu wa kujiamini na kuthubutu kutumia fursa zinazojitokeza,” amesema Angela.
Amesema pia mafunzo kuhusu matumizi ya teknolojia ya akili unde (AI) yamewasaidia wanafunzi kujifunza namna ya kupata maarifa kwa urahisi kupitia vitabu na vyanzo mbalimbali vya mtandaoni, ikiwemo vile ambavyo havipatikani katika maktaba za kawaida.
“Teknolojia hii imetupa fursa kubwa ya kujifunza, lakini pia imetukumbusha kuwa ubunifu na fikra za binadamu bado ni muhimu katika kutatua changamoto na kuibua mawazo mapya,” amesema Angela.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Dk Kedmon Mapana amesema Tanzania Bara ina vijana milioni 20.6 sawa na asilimia 34.4 ya wananchi wote, kundi ambalo lina nafasi kubwa ya kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha vijana kupitia uchumi wa kidijitali, mikopo ya maendeleo na programu za ubunifu ili kuongeza ajira na fursa za kujiajiri.
Dk Mapana amesema Serikali imetenga Sh200 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha vijana, wanawake na makundi mengine maalumu kiuchumi, huku ikiendelea kusimamia mikopo ya asilimia nne ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa vijana.