Vijana watakiwa kuchangamkia taka

Muktasari:

  • Mgitu amesema mnyororo wa thamani katika taka ni eneo linaloweza kutengeneza faida kubwa ikiwa watu watawekeza kwa makini, huku akitoa wito kwa vijana wa kitanzania waliopo mitaani kuchangamkia fursa hiyo akisema kuwa taka ni mali.

Dar es Salaam. Wakati vijana wengi wakilalamika kuhusu ukosefu wa ajira hivyo kujikuta mitaani wakilia njaa, fursa katika mnyororo wa thamani wa taka, zinazidi kuongezeka huku wakitakiwa kuzichangamkia.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Novemba 24, 2023 na Zephania Mgitu, Meneja wa Miradi kutoka Elico Foundation, wakati wa mafunzo yaliyowakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira jijini Dar es Salaam.

Mgitu amesema mnyororo wa thamani katika taka ni eneo linaloweza kutengeneza faida kubwa ikiwa watu watawekeza kwa makini huku akitoa wito kwa vijana wa Kitanzania waliopo mitaani kuchangamkia fursa hiyo akisema taka ni mali.

“Ikiwa idadi ya watu inazidi kuongezeka kwa kasi kubwa, halafu uendelezaji wa miundombinu na udhibiti wa taka ukawa bado sio mzuri, maana yake tutakuja kukuta tunatengeneza jiji ambalo usafi ni changamoto kwake,” amesema na kuongeza:

“Kuna watu wanahangaika sana kutafuta kazi za kufanya, kwa Dar es Salaam taka ni fursa kubwa sana, tumia akili yako vizuri. Kama hautaki kukusanya unaweza ukasajili kampuni ambayo itakuwa inasafirisha hizo taka,” amesema Mgitu.

Tabu Ally anayejihusisha na ukusanyanyi wa majani na kuyageuza kuwa mbolea amesema kuwa mafunzo hayo yaliyotolewa na shirika hilo lisilo la kiserikali, yatawasaidia kuongeza ujuzi na kujenga uwezo kwenye biashara zao, huku akisihi elimu izidi kutolewa kwa vijana kwani ni changamoto inayowakabili.

Kwa upande wake, Hilal Zahor anayejihusisha na ukusanyaji wa taka chuma na plastiki, amezungumzia changamoto zinazoikabili biashara hiyo akisema gharama za vibali vya ukusanyaji taka ni kubwa hali inayosababisha watu wengi kukata tamaa na kuhamia kwenye maeneo mengine.

Naye, mdau kutoka Taasisi ya Mazingira Plus, Tryphone Richard amesema mafunzo hayo yatawasaidia wao kama wanaharakati wa mazingira kujifunza mambo mbalimbali kisha kupeleka elimu hiyo kwenye jamii inayowazunguka ili kusaidia kuondoa usambaazaji hovyo wa taka.

Mradi huo umeanzishwa na Mayors Migration Council ambapo umelenga kuongeza fursa katika mnyororo wa thamani wa taka.