Vijiji 20 vyapatiwa mbuzi wa maziwa kukabili udumavu

Baadhi ya wanufaika wa msaada wa mbuzi wa maziwa kutoka Kijiji cha Uhelela, wilayani Bahi, wakiwa na mbuzi wao baada ya kukabidhiwa na shirika la Save the children. Picha na Rachel Chibwete.

Muktasari:

Tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano nchini ni asilimia 30.

Bahi. Ili kukabiliana na tatizo la udumavu na utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano Halmashauri ya Wilaya ya Bahi imetoa msaada wa mbuzi wa maziwa kwa kina mama wenye watoto walio chini ya miaka mitano.

Msaada huo umetolewa na Shirika lisilo la kiserikali la Save the children leo Jumamosi Machi 2, 2024 kupitia mradi  wa Lishe yangu afya yangu.

Jumla ya mbuzi wa maziwa 128 wamegawiwa kwa kaya masikini.

Ofisa mifugo, kilimo na uvuvi wa Wilaya ya Bahi, Siwajibu Selemani amesema mradi huo wa mbuzi wa maziwa utasaidia kaya hizo masikini kupambana na udumavu na utapiamlo kwa watoto walio chini ya miaka mitano pamoja na wajawazito.

"Tunataka mtumie msaada huu kuboresha afya za watoto na wajawazito kwa sababu kama watoto hawa watakosa lishe bora watapata utapiamlo ambao unaweza kuzuilika kwa kuwapa chakula bora ikiwemo maziwa ya mbuzi," amesema Siwajibu.

Amesema wataalamu wa mifugo wa halmashauri watawasaidia wanufaika hao kwenye matibabu pindi watakapopata magonjwa na kuwataka kuwahudumia na kuwatunza ili walete manufaa yaliyokusudiwa.

Chausiku Yohana, mnufaika wa mradi huo amesema maziwa yatakayopatikana kutokana na mbuzi hao yatamsaidia kuboresha lishe ya watoto wake na kujiongezea kipato kwa kuyauza.

Chausiku ambaye ni mama wa watoto watatu wote wakiwa chini ya miaka mitano amesema awali alikuwa anashindwa kumudu gharama za kununua maziwa ambayo yanauzwa Sh1,000 kwa lita moja.

Amesema msaada huo utamsaidia yeye na majirani zake kwani watoto watakaotokana na mbuzi hao atawagawia.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Uhelela kilichopo Kata ya Mlowa wilayani Bahi, Mosi Ndahani ambaye kijiji chake kimepata msaada wa mbuzi sita amesema uongozi wa kijiji hicho utahakikisha malengo ya Serikali ya kugawa mbuzi hao yanafikiwa.

Amesema mbali ya maziwa, wanufaika watapata mbolea  itakayotumika kustawisha mazao yao.

Amewaonya kuhusu kuchinja mbuzi hao kwa kuwa hairuhusiwi na si malengo ya msaada huo.

Mariamu Mwita, Meneja mradi wa Shirika la Save the children amesema vijiji 20 wilayani Bahi vitanufaika na mradi huo kwa kila kijiji kupata mbuzi sita.

Kati ya idadi hiyo, majike ni matano na beberu mmoja.

Amesema mbuzi hao wakilishwa vizuri wana uwezo wa kutoa lita nne za maziwa kwa siku, asubuhi mbili na jioni mbili.

"Maziwa yatakayopatikana watatumia kama lishe kwenye familia zao lakini yatakayobakia watauza na kujiongezea kipato maana tumewashauri pia kulima bustani kwa ajili ya kupata mbogamboga kwa lishe ya watoto wao na wao wenyewe," amesema Mariam.

Kuhusu udumavu

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa kuzima Mwenge wa Uhuru, Oktoba 14, 2023 aliwataka wananchi kutekeleza maelekezo ya wataalamu kuhusu lishe, akisema licha ya jitihada kubwa za kukabiliana na changamoto hiyo bado hali hairidhishi.

Aliwaagiza wakuu wa mikoa kuendelea na utekelezaji wa mikataba ya lishe waliyoisaini.

Alisema takwimu za udumavu zinaonyesha asilimia 28 ya wanawake waliopo katika hatua ya kujifungua wana upungufu wa damu, huku asilimia 32 wana uzito uliozidi.

Rais alisema tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ni asilimia 30 na uzito pungufu ni asilimia 12, ukondefu asilimia tatu na uzito uliopitiliza asilimia nne.

“Kiwango cha udumavu cha asilimia 30 ni kiashiria cha hali mbaya ya lishe kwa mujibu wa viwango vya WHO (Shirika la Afya Duniani).

Mikoa inayoongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu na udumavu zaidi ya wastani wa kitaifa ni Iringa asilimia 56.9. Ikifuatiwa na Njombe (50.4), Rukwa (49.8), Geita (38.6) Ruvuma (35.6), Kagera (34.3), Simiyu (33.2), Tabora (33.1), Katavi (32.2), Manyara (32), Songwe (31.9) na Mbeya (31.5).