Vijiji 54 kupata maji ya visima

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela (wapili kulia) akiangali mtambo wa kuchimba visima virefu unavyochimba kisima katika kijiji cha Ntono kata ya Bukoli wilaya ya Geita.

Muktasari:

Wakazi wa Vijiji 54 kutoka Wilaya tano za Mkoa wa Geita wako mbioni kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji baada ya Serikali kutoa Sh1.2 bilioni ya kuchimba visima virefu kwenye vijiji hivyo.

Geita. Wakazi wa Vijiji 54 kutoka Wilaya tano za Mkoa wa Geita wako mbioni kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji baada ya Serikali kutoa Sh1.2 bilioni ya kuchimba visima virefu kwenye vijiji hivyo.

Mradi huo unaotarajiwa kutekelezwa katika bajeti ijayo ya 2023/24 itawezesha visima virefu 54 kuchimbwa na kutimiza adhma ya Serikali ya kumtua mama ndoo kichwani.

Akizungumza Juni 2, 2023 wakati wa uzinduzi wa mtambo wa kuchimba visima virefu uliofanyika katika Kijiji cha Ntono Kata ya Bukoli Wilaya ya Geita, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Jabir Kayilla amesema mradi huo ni sehemu ya fedha za Uviko 19.

Kayilla amesema uchimbaji wa visima hivyo ni matokeo ya Serikali kutoa mtambo wa kuchimba visima virefu wenye gharama ya Sh600 milioni, mbali na kuchimba Ruwasa pia itafanya kazi ya kusambaza maji hadi kwenye makazi ya wananchi.

“Mtambo huu ni sehemu ya mitambo iliyotolewa nchi nzima na Serikali ya awamu ya sita ambazo ni fedha za Uviko 19 na Rais alielekeza Wizara ya maji ambayo ni wanufaika wa fedha hizo kuhakikisha wanajenga miradi mikubwa ya maji kwenye maeneo yenye changamoto ya maji pamoja na kuchimba visima na sisi leo tunazindua kwenye kijiji hiki,”amesema Kayilla

Amesema Kijiji cha Ntono ambacho uchimbaji wa kisima umeanza wananchi zaidi ya 5, 800 watanufaika kwa kupata maji safi na salama ambapo pia Ruwasa watajenga miundombinu ya kusambaza maji ikiwemo ujenzi wa tanki kubwa la maji ,mtandao wa mabomba na kuweka vituo vya kuchotea maji.

Akizindua mtambo huo Mkuu wa Mkoa wa GGeita Martine Shigela amesema kukosekana kwa maji kunasababisha shughuli za maendeleo zishindwe kutekelezwa kutokana na wananchi kutumia muda mwingi kutafuta maji.

Shigela amewataka wananchi kushirikiana na Serikali kukamilisha miradi hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa ardhi kwa ajili ya kujenga matanki ya maji, kupitisha mabomba na kuitaka Ruwasa kuhakikisha maji yatakayopatikana hayauzwi kwa zaidi ya Sh40 kwa ndoo ya lita 20.

Mkazi wa kijiji hicho, Aziza Masood amesema kutokana na changamoto ya maji hasa kipindi cha kiangazi hulazimika kutumia maji ya madimbwi ambayo sio salama kwa afya zao na kusababisha kuugua magonjwa ya matumbo.