Vijiji kukabidhiwa hati miliki za kimila
Muktasari:
Wapimaji wasema mashamba ya mpunga yanapunguza kasi ya upimaji hivyo hulazimika kuchukua muda mrefu
Morogoro. Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi (NLUPC), imeanza kutoa hati za kimila kwa vijiji ambavyo vimeshapimwa na kupangiwa matumizi bora ya ardhi nchini, ili kuondoa migogoro.
Mpango umekalimika baada ya Rais John Magufuli kuiagiza NLUPC kupima, kupanga na kumilikisha vijiji 7,500 ifikapo mwaka 2020. Ikiwa ni wastani wa vijiji 1,500 kwa mwaka.
Tume hiyo kwa kushirikiana na asasi za kiraia, mashirika yasiyo ya serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi ikiwamo Care International Tanzania, Oxfam, Chama cha Wafugaji Tanzania, Chuo Kikuu cha Ardhi, Tamisemi na MALF tayari wameanza kutekeleza agizo hilo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Takwimu za Kampuni ya City Plan, inayohusika na upimaji ardhi, zinaonyesha kuwa vipande vya ardhi 1,171 tayari vimepimwa na kugawiwa kati ya 2,700 vilivyohakikiwa katika vijiji vya Hambeti na Dihombo, Wilaya ya Mvomero hadi Septemba 5.
Kati ya vipande hivyo, 736 viligawiwa Dihombo na 435 vya Hembeti.
Akizungumza juzi na wanakijiji wa Dihombo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe alisema kazi hiyo itasaidia kuondoa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji.
Dk Kebwe alisema elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa wanavijiji ili kujua umuhimu wa kushiriki katika upimaji na umilikishwaji ardhi, hatua itakayoondoa migogoro.
Kaimu Mkurugenzi wa NLUPC, Dk Stephen Nindi alisema ofisi yake inafanya kazi kwa ukaribu na mashirika yasiyo ya Serikali, lengo ni kupima vijiji 7,500 ifikapo mwaka 2020.
Dk Nindi alisema vifaa vya kupimia ardhi RTK (Real Time Kinematic) vitano vinahitajika kwa sasa ili kukamilisha jukumu hilo kwa wakati uliopangwa.
“Mpaka sasa tuna vifaa vya RTK viwili pekee. Tunahitaji vitano ili kufanya kazi haraka na kukamilisha kwa kipindi kifupi, kifaa kimoja kinagharimu Sh80 milioni,” alisema Dk Nindi.