Vijiji vitano, vitongoji 41 kuhamishwa hifadhi ya Usangu

Muktasari:

Serikali imedhamiria kuondoa vijiji vitano na vitongoji 41 kutoka katika vijiji 14 ili kupisha eneo la hifadhi ya Usangu kwa lengo la kutunza na kulinda ardhi oevu pamoja na vyanzo vya kupokea na kutiririsha maji katika mito mbalimbali.

Dar es Salaam. Vijiji vitano na vitongoji 41 vilivyopo katika vijiji 14 ikiwemo sehemu ndogo ya kitongoji cha Magwalisi kilichopo mamlaka ya mji mdogo wa Rujewa wilayani Mbarali vitahamishwa na Serikali ili kupisha eneo la hifadhi.

Uhamisho huo pia utavikumba vitongoji vitatu katika kijiji cha Lualaje wilayani Chunya.

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Oktoba 25, 2022 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula katika mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo la Ubaruku Mbarali wakati Kamati ya mawaziri nane wa wizara za kisekta walipofanya ziara kwenye eneo la mto ruaha na mnazi katika kijiji cha Mwanavala eneo lililopo kwenye hifadhi.

Amesema uamuzi huo wa Serikali unalenga kutunza na kulinda ardhi oevu pamoja na vyanzo vya kupokea na kutunza maji yanayotiririka kutoka mito mbalimbali.

Waziri Mabula amevitaja vijiji vitakavyoondoka kwa asilimia 100 kuwa ni Luhanga, Madundasi, Msanga, Iyala na Kalambo vyenye idadi ya watu 21,252 na kusisitiza watu wa maeneo hayo wanatakiwa wasiwepo na usajili wa vijiji hivyo kufutwa.

“Katika shughuli hii wenye kulipwa fidia watalipwa na wale wasiostahili wataondoka kama walivyokuja na lengo la Serikali ni kuwa na urithi wa watu wote,’’ amesema Dk Mabula.

Amesema Serikali imeridhia vijiji 15 vyenye ukubwa wa hekta 74,324.12 na ranchi ya Usangu ya NARCO kuendelea kubaki huku vijiji vyote vinavyopakana na hifadhi ya Ruaha kufanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi.

Uhifadhi wa Bonde la Usangu ulianza mwaka 1953 wakati eneo likijulikana kama pori tengefu la utengule likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 500 kwa lengo la kuhifadhi bioanuwai katika ardhi oevu ya ihefu.

Kutokana na uharibifu mkubwa wa  mazingira na vyanzo vya maji uliofanyika miaka ya 1990 serikali iliamua kupandisha hadhi pori tengefu la Utengule na kuwa pori la akiba la Usangu likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 4148 kwa tangazo la Serikali namba 436A la tarehe 24 julai 1998 kabla ya Serikali kuja na mkakati mwingine mwaka 2006.