Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vilio wanyama wanavyoharibu mazao, kujeruhi wananchi-1

Kilimanjaro, Singida. Ukistaajabu ya Musa, utaona ya Firauni,  ndivyo unavyoweza kueleza hali inayowakumba wakazi wa maeneo ya Same, mkoani Kilimanjaro kutokana na tembo kuwa tatizo kubwa, wakifanya vitendo visivyotarajiwa na binadamu.

Wanyama hao sasa wanazurura mitaani, wakila vyakula kama maziwa, matikiti, pumba za mahindi, kuharibu mashamba na hata kula katani.

Ripoti maalumu ya Mwananchi imebaini athari kubwa zinazotokana na wanyama hao katika mikoa ya Kilimanjaro na Singida. Tembo si tu wanaharibu mazao, bali pia wanasababisha vifo na majeraha kwa wakazi wa maeneo hayo. Fisi pia wamekuwa tishio, wakijeruhi wananchi.

Miongoni mwa waliokumbwa na shambulio la fisi ni Emmanuel Jackson, mkazi wa Doroto, Wilaya ya Manyoni, Julai 14, akiwa anakwenda kuchota maji bwawani.

Vilio wanyama wanavyoharibu mazao, kujeruhi wananchi-1

Anasema fisi alimvamia na kumjeruhi mkono baada ya kupambana naye kwa nusu saa. Aliokolewa na wananchi, huku akiwa amejeruhiwa na maeneo mengine kama mgongoni.

Alilazwa hospitalini kwa siku 16, akifanyiwa upasuaji mara nne kwa gharama ya Sh1.8 milioni. Anaiomba Serikali na wadau kumsaidia kupata matibabu zaidi.

Akizungumzia maisha ya wasiwasi kwa kuhofia kukutana na wanyama hao, Anastazia Juma, mkazi wa kitongoji cha Mgulu wa pembe, Kijiji cha Doroto Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida, anasema wanapata changamoto ya kuvamiwa na tembo nyumbani mara kwa mara.

“Visima vya maji vilivyochimbwa karibu na makazi vimekuwa kivutio kikubwa kwa tembo ambao sasa wamekuwa wakizurura mitaani kama wanyama wa kufugwa,” anasema.

Anastazia anaeleza jinsi watoto wanavyolazimika kulala mbali na nyumbani wanapokutana na tembo njiani. Baba yake pia alinusurika kuuawa na kundi la tembo alipokuwa akirejea nyumbani usiku.

“Kilimo chetu kimeathirika sana. Mwaka jana tulilima ekari nne za mahindi, lakini hatukuvuna hata punje moja baada ya tembo kula kila kitu," anasema Anastazia.

Pia anabainisha kuwa tembo hao wamekuwa wakivamia hata minada na kusababisha taharuki, licha ya juhudi za wanyamapori kuwafukuza.


Vifo

Agosti 11, 2024, Mrisho Shabani, maarufu kama Mwiluu, aliuawa na tembo karibu na nyumbani kwake. Rukia Hamisi, mjane wa marehemu, anaeleza jinsi tembo walivyomkanyaga mumewe bila huruma, wakivunja mifupa yote na kuharibu vibaya mwili wake.

Familia hiyo sasa inakabiliwa na maisha magumu, hasa baada ya kuachwa na watoto sita wenye umri mdogo. Rukia anaiomba Serikali kutimiza ahadi ya kutoa fidia kwa familia yake ili kusaidia malezi ya watoto hao.


Kilimo chashindikana

Hamisi Babasungu, aliyeishi kijiji cha Doroto tangu mwaka 1984, anasema amekuwa akipata hasara kubwa kutokana na tembo kula mazao yake, akieleza kuwa hali hiyo imeongezeka katika miaka mitano ya karibuni.

“Ningepata Sh2.2 milioni kutoka kwenye shamba langu la ekari saba, lakini yote yanaishia mdomoni mwa tembo. Tembo hawa wamekuwa sugu. Ukimpigia tochi, anakupa mgongo na kuendelea na shughuli zake,” anasema Hamisi.

Wananchi wa Wilaya ya Same wanakumbwa na madhila kutokana na uharibifu unaosababishwa na wanyama, hasa tembo, wanaovamia mashamba na kuharibu mazao.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kandoto, Theopista Seleman, anasema kitongoji hicho kipo umbali wa kilomita 25-30 kutoka Hifadhi ya Mkomazi na kinakumbwa na uharibifu mkubwa, hasa na tembo. “Malalamiko yangu ni kwamba malipo ni kidogo mno, mtu akiharibiwa kuanzia nusu eka halipwi hadi iwe eka moja,” anasema Seleman.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisima, Gabriel Mzava, anasema malipo ya wanyama wanaoharibu mazao ni ya chini, inapaswa kutungiwa mipango ya miradi inayowanufaisha wananchi, kama matumizi ya mizinga ya nyuki kufukuza tembo.

“Hiyo sehemu wanayopitia tembo ikizibwa hawatafika kwa wananchi,” anashauri Mzava.

Samwel Mbugu, anasema juhudi za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) hazitoshi kutokana na upungufu wa magari na rasilimali. “Walikuja nyumbani kwangu, walikula kila kitu, walirudi Mbugu, akionyesha hali ngumu wanayoishi.

Rajabu Mgonja kutoka Kijiji cha Masandare anasema tembo wameharibu mabomba ya maji na mazao yao.

“Tembo wanang’oa mabomba ya maji kila kukicha, wanashirikiana kufukia mashimo tuliyochimba,” anasema Mgonja.

Athumani Juma, mkazi wa Masandare, anasema: “Hatukuwa na shida na wanyama, lakini sasa hali ni mbaya. Miti inang’olewa na mazao yanaharibiwa.”

Wanyama hao hawahatarishi tu mazao, bali pia miundombinu ya kijamii. Halima Selemani, Mwenyekiti Msaidizi wa Shule ya Msingi Kishaa - Same, anasema tembo wameharibu miundombinu ya maji ya shule.


Viongozi watoa neno

Mwenyekiti wa Kijiji cha Masandare, Bakari Mshana, anashauri Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) na Tanapa kuongeza wafanyakazi, akidai waliopo hawatoshi na matatizo ya wanyama yanatokea kila mara maeneo karibu yote wilayani Same.

“Mkulima akiharibiwa mazao yake alipwe kifuta jasho kwa wakati na kinacholingana na mazao yaliyoharibiwa badala ya kuangalia ni nusu eka au eka moja," anasema.

Ofisa Wanyamapori Wilaya ya Same, Thomas Katunzi, anasema kuwa tembo wana uwezo mkubwa wa kukumbuka njia zao, hivyo anasisitiza "uwezo wa tembo kukariri ni mkubwa anashika namba tatu, wa kwanza binadamu, wa pili wanyama jamii ya sokwe na wa tatu ni tembo."

Katunzi pia anafafanua kuhusu viwango vya malipo kwa wananchi, akieleza kuwa "viwango vya pole vinatofautiana, kwanza zilizokuwa zinalipwa ekari tano hazilipwi chini ya hizo na unaangalia umbali kutoka mpaka wa hifadhi ili kuzuia shughuli hizo. Chini ya mita 500 mtu akiharibikiwa mazao yake halipwi. Lakini baadaye ikawa wanalipwa mkono wa pole kuanzia eka moja."

Naye Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Dk Mashinji, anasema changamoto za wanyama kuvamia makazi ya watu zinasababishwa na mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa vyanzo vya maji, na kupungua kwa wanyama wawindaji.

“Binadamu wameharibu vyanzo vya maji, yale maeneo yaliyokuwa yanatiririsha maji kwenye hifadhi hayana maji tena, wanyama wanalazimika kuyatafuta nje ya hifadhi,” anasema.

Anabainisha kuwa tembo sasa wanaweza kunusa nafaka na kuvamia nyumba kutafuta chakula. “Tembo anajua harufu ya nafaka na ana uwezo wa kunusa kwa umbali mrefu. Anaweza kuvunja nyumba na akishakula, anatulia,” anasema.

Dk Mashinji pia anakosoa matumizi mabaya ya ardhi, akisema: “Mtu wa kawaida anamiliki eka 1,000, anazifanyia nini? Tunahitaji mkakati wa matumizi bora ya ardhi ili kuondoa malalamiko haya.”

Anasisitiza kuheshimu hifadhi za wanyama kama ilivyokusudiwa na Baba wa Taifa.


Itaendelea kesho kuona madhila kwa wakazi pembezoni mwa ziwa Victoria. Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.