Viongozi wa dini: Serikali ipige marufuku pombe za kienyeji Kilimanjaro

Askofu mstaafu wa TAG Kilimanjaro na Mkurugenzi wa New Life Foundation, Glorious Shoo akizungumza wakati akitambulisha kongamano la siku 5 la Kimataifa la kuombea mvua na ukame unaoenedelea katika uwanja wa soko la Maimoria, Manispaa ya Moshi. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kupiga marufuku pombe za kienyeji zinazotumia mazao ya chakula hasa mahindi na ndizi kwa kuwa zinapunguza kiwango kikubwa cha chakula katika kipindi hiki cha ukame.
Moshi. Viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kupiga marufuku pombe za kienyeji zinazotumia mazao ya chakula hasa mahindi na ndizi kwa kuwa zinapunguza kiwango kikubwa cha chakula katika kipindi hiki cha ukame.
Pamoja na kupiga marufuku pombe hizo, wameiomba serikali kuweka mpango madhubuti wa kupunguza makali ya mfumuko wa bei za vyakula kwa kuweka ruzuku kwenye chakula ili kuwanusuru wananchi na baa la njaa.
Hayo yamesemwa leo Novemba 10, 2022 na Askofu Mstaafu wa TAG Kilimanjaro, na Mkurugenzi wa New Life Foundation, Glorious Shoo wakati akitambulisha kongamano la siku 5 la Kimataifa la kuombea mvua na ukame unaoendelea katika Uwanja wa Soko la Maimoria, Manispaa ya Moshi.
Kongamano hilo linawahusisha wahubiri wa Kimataifa, kutoka Mataifa ya Norway, Finland, Ujerumani na Tanzania.
"Ni vizuri tukaendelea kuhimiza watu kutumia kwa uangalifu chakula kilichopo ili tuweze kuhifadhi chakula kwa wakati huu wa ukame, ombi langu ni kuomba serikali kupiga marufuku pombe za kienyeji zinazotumia mazao ya chakula.
"Ziko pombe nyingi za kienyeji ambazo hazimsaidii mtu yeyote lakini ukweli bado zinapunguza kiwango kikubwa cha chakula kwa kutengenezea pombe za kienyeji hasa zinazotumia mahindi na ndizi," amesema.
Pamoja na mambo mengine amesema kwa miezi mitatu sasa vyakula vimekuwa vikipanda bei bila kushuka na ukitarajia ya kwamba mavuno wakati yanapofanywa kwenye eneo fulani labda bei zingeshuka, haijatokea na imeendelea kubakia juu.
"Kama serikali ilivyoweka ruzuku tunaamini inaweza likafanyika jambo hilo kabla hali haijawa mbaya zaidi, ni vizuri tukaendelea kuweka restriction (zuio) kwenye uuzaji holela wa chakula na kwenye matumizi holela ya chakula," amesema.
" Huu ni wakati wa serikali kusimama imara na kupiga marufuku pombe hizi kwa sababu hali itakuwa mbaya zaidi kama chakula kilichoko kitatumika kwa matumizi yasiyokuwa ya lazima, hususani pombe ambayo ina athari nyingi katika familia na katika jamii zetu," amesema.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste ya Mkoa wa Kilimanjaro (CPCT), Askofu Cleopa Kweka, amesema ukame umeathiri maeneo mengi hapa nchini na kupelekea wananchi kukosa chakula huku mifugo ikifa kwa kukosa malisho.
"Sasa hivi tunahitaji ushirikiano mkubwa wa kuliombea Taifa letu. Ninaamini neno la Mungu ni moja ya msaada mkubwa unaoleta amani, utulivu na baraka, tunaona jinsi watu wana njaa, mifugo inakufa hali hii ni mbaya ukiangalia maeneo mengi ya nchi hii kuna njaa kali," amesema Kweka.
Kiongozi wa jopo la wahubiri hao wa kimataifa, Mwinjilisti Daniel Smenes wa Huduma ya Jesus to All Nations, amesema baadhi ya nchi sasahivi zimekumbwa na ukame unaotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kulrta athari kubwa kwa watu na wanyama.
"Tunafahamu mabadiliko ya tabianchi na janga la ukame na ninaamini ya kwamba kwenye hilo si suala la maombi tu, kila mmoja kwa wakati wake tuwahimize watu waweze kuyatunza mazingira kwa sababu hilo halihitaji maombi. Kimsingi ni watu wajali mazingira yao na kuzuia athari ambazo zinazoweza kuleta ukame," amesema